Frank Mvungi- MAELEZO, Dodoma
Mradi wa maji wa Kimbiji na Mpera kuanza kuwanufaisha Wananchi baada ya kukamilika kwa awamu ya pili ambayo itahusu ujenzi wa miundombinu ya kusambaza maji ambapo utaanza kutekelezwa katika bajeti ya mwaka 2018/2019.
Akijibu swali la Mbunge wa viti maalum Mhe. Lucy Simon Magereli aliyeta kujua ni lini mradi huo utakamilika ili kuondoa adha kwa wananchi wa Kigamboni ambao wengi wao wanatumia visima vifupi ambavyo si salama, Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhe. Jumaa Aweso amesema kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kuwa inaondoa adha ya upatikanaji wa maji kwa Wananchi wa maeneo mbalimbali ikiwemo Kigamboni.
“Serikali imeanza kutekeleza miradi mbalimbali minne (4) ya uboreshaji wa huduma ya maji kwa mpango wa muda mfupi kwa wakazi wa Kigamboni,” alisema Mhe. Aweso
Akifafanua Mhe. Aweso amesema kuwa miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa mtandao wa mabomba, kusambaza maji ya kutoka Ruvu chini kupitia bomba linalovuka bahari eneo la Kurasini kwenda Kigamboni ili kusambaza maji maeneo ya Tipper, Chuo cha Mwalimu Nyerere na Kigamboni Ferry kuelekea Mji Mwema.
Ameitaja miradi mingine kuwa ni ujenzi wa miundo mbinu ya kusambaza maji kutoka visima vya Vijibweni kuelekea maeneo ya ofisi mpya ya Manispaa ya Kigamboni na kuendeleza kisima cha mita 600 cha Kisarawe ili kufikisha maji Kibada na maeneo ya Viwanda (Light Industry Zone) la Kimbiji.
Akizungumzia mikakati ya Serikali kumaliza ujenzi wa miundo mbinu ya Maji katika Kata za Igowole, Nyololo, Mninga, Mtambula, Nyigo na Idunda, Mhe. Aweso amesema kuwa Kata za Igowele, Nyololo, Mninga, Mtambula na Idunda zina jumla ya vijiji 23 vyenye wakazi takribani elfu 69,119.
Mhe. Aweso amesema kuwa, katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi imetenga Shilingi Bilioni 2.67 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji vijijini zikiwemo kata hizo ambapo hadi sasa usanifu wa kina umekamilika na uandaaji wa makabrasha ya zabuni unaendelea na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Mei, 2018.
Kazi hizo zinatekelezwa na Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Iringa (IRUWASA) kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi na Sekretarieti ya Mkoa wa Iringa.
Aidha amesema, Ujenzi wa miundo mbinu ya miradi hiyo ya maji unatarajiwa kuanza katika mwaka wa fedha 2018/2019 ambapo Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 2.25 kwa ajili ya miradi ya maji vijijini katika halmashauri ya Wilaya ya Mufindi zikiwemo Kata za Igowole, Nyololo, Mninga, Mtambula, Nyigo na Idunda.