Tanzania itatekeleza Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) ambao chini ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa lengo la kupanga, kupima, kumilikisha na kutoa hati miliki za ardhi kuongeza usalama wa milki za ardhi nchini.
Akihitimisha Kikao Kazi cha Asasi za Kiraia ambacho kimefanyika kwa siku mbili hivi karibuni jijini Dodoma, Mratibu Msaidizi wa Mradi huo, Dkt. Upendo Matotola amesema mradi huo unatumika kama mfano kwa ulimwengu na kuwasisitiza washiriki hao kuijenga nchi kwa pamoja ili kujenga taswira njema ya Tanzania kimataifa.
“Tunajua kabisa tunapopanga, tunapopima, na kumilikisha vipande vya ardhi, Uchumi wetu unaongezeka kwa sababu ardhi iliyopangwa na kupimwa inaongezeka thamani na inapoongezeka thamani, shughuli za kiuchumi nazo zinaongezeka”, amesema Dkt. Upendo.
Katika kutekeleza mradi huo, Dkt. Upendo amesema kuwa Serikali inatoa kipaumbele kwa sekta binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali na mashirika ya kijamii katika kutekeleza masuala ya ardhi na kusisitiza kuwa Serikali itabaki na jukumu la kujenga uwezo, mazingira wezeshi, utawala na usimamizi wa ardhi nchini.
Akizungumza na washiriki hao, Dkt. Upendo amesema, “Sisi wote ni wazalendo, tunapenda mradi huu uendelee kutekelezwa vizuri kama ulivyokusudiwa kuleta matokeo chanya yenye tija kwa taifa letu ili kutoa fursa kwa miradi mingine kutekelezwa hapa nchini, tunaposema vibaya kuhusiana na mradi, tunajichafua wenyewe.”
Aidha, amewasisitiza washiriki hao kuwa wafanisi kwani mradi huo unategemea ushiriki wao mzuri kwa kutoa utaalamu wao kwa kufanya kazi kwa uaminifu na uadilifu kwa uzalendo kwa kutanguliza maslahi ya taifa lao.
Kwa upande wao mshiriki wa kikao kazi hicho, Bw. Innocent Jaji kutoka Maswa na Bi. Mariam Mohamed kutoka Mvomero wamesema kuwa Asasi za Kiraia zina jukumu la kushirikiana na serikali katika kutelekeza mradi huo kwa kutoa elimu ya masuala ya ardhi makundi maalumu wakiwemo wanawake, wazee, watoto na watu wenye ulemavu wapate haki zao katika umiliki wa ardhi.
Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) ambao unatekelezwa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Dunia umeanza kutekelezwa mwaka 2022 na unatarajiwa kukamilika 2027 ambapo jukumu lake ni kurasimisha ardhi kwa wananchi katika maeneo ya mijini na vijijini.