Uwekezaji katika teknolojia ya kisasa, utaalamu wa huduma za kibingwa na kibobezi na utekelezaji wa miradi ya kimkakati umeiwezesha Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) kupunguza kwa kiasi kikubwa rufaa za kupeleka wagonjwa nje ya nchi, hatua inayookoa fedha za kigeni na kuimarisha huduma za afya nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Mhe. Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Idara ya Habari- MAELEZO, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mtumba jijini Dodoma.

Dkt. Ulisubisya amesema katika kipindi cha mwaka mmoja pekee, wagonjwa 2,228 wamepatiwa huduma za kibobezi ndani ya nchi, huduma ambazo hapo awali zilihitaji safari za nje zenye gharama kubwa kwa wagonjwa na taifa kwa ujumla.
Amefafanua kuwa katika eneo la huduma za ubongo na mishipa ya damu, MOI sasa inatekeleza upasuaji na uchunguzi wa mishipa ya damu kwenye ubongo bila kufungua fuvu, teknolojia ya kisasa inayopunguza hatari, maumivu na muda wa kupona kwa mgonjwa.
“Kwa miaka mingi, wagonjwa wenye matatizo ya ubongo, mgongo na mifupa walilazimika kusafiri nje ya nchi kutafuta matibabu ya kibingwa. Safari hizo zilikuwa na gharama kubwa, usumbufu kwa familia na mzigo kwa taifa. Leo, simulizi hiyo inabadilika kupitia uwekezaji wa teknolojia na utaalamu wa madaktari bingwa,” amesema Dkt. Ulisubisya.

Aidha, amebainisha kuwa huduma za matibabu ya kiharusi kupitia mishipa mikubwa ya damu (interventional stroke treatment) zimeokoa maisha ya wagonjwa wengi waliokuwa katika hatari ya kupooza au kupoteza maisha, na hivyo kuongeza matumaini kwa wananchi wanaohitaji huduma hizo hapa nchini.

Hatua hizo zinaifanya MOI kuwa miongoni mwa taasisi zenye uwezo mkubwa wa kibobezi barani Afrika na duniani, huku zikichangia utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050 inayotoa mwelekeo wa nchi kujitegemea katika sekta ya afya na kuimarisha upatikanaji wa huduma bora kwa Watanzania.