Serikali kupitia Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) imepiga hatua nyingine muhimu katika maboresho ya sekta ya afya baada ya kuanzisha rasmi matumizi ya Akili Unde (Artificial Intelligence – AI) katika utoaji wa huduma za upasuaji na matibabu ya kibobezi.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Februari 2, 2026 katika Ukumbi wa Idara ya Habari – MAELEZO, Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dkt. Mpoki Ulisubisya, alisema teknolojia hiyo inalenga kuongeza usahihi katika uchunguzi, kupanga matibabu na kuboresha utekelezaji wa upasuaji.

Ameleza kuwa kwa muda mrefu taasisi hiyo imekuwa ikitumia mbinu za kawaida katika uchunguzi na matibabu, ambazo wakati mwingine zilikuwa zikichukua muda mrefu na kuongeza siku za wagonjwa kulazwa hospitalini.
"Kupitia AI, madaktari sasa wana uwezo wa kufanya uchambuzi wa haraka na wa kina wa vipimo mbalimbali, hivyo kufanya maamuzi sahihi kwa wakati" amesema Balozi Dkt. Ulisubisya.
Dkt. Ulisubisya alifafanua kuwa tayari madaktari wameanza kutumia teknolojia hiyo katika afua ya upasuaji wa mgongo kwa njia ya matundu madogo (minimally invasive surgery), ambayo hutoa matokeo yanayolingana na upasuaji wa kawaida wa kufungua, lakini kwa maumivu madogo na muda mfupi wa kupona.

Ameongeza kuwa matumizi ya akili unde yanasaidia kupunguza muda wa upasuaji, kupunguza hatari zinazoweza kujitokeza wakati wa upasuaji na kuongeza kiwango cha mafanikio ya matibabu, hususan kwa wagonjwa wanaohitaji huduma za mifupa, ubongo na mishipa ya fahamu.
Hatua hiyo ni sehemu ya mkakati mpana wa Serikali wa kuimarisha matumizi ya teknolojia za kisasa katika sekta ya afya, kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na za kisasa ndani ya nchi.