Mkutano wa 27 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi unaendelea katika Jiji la Sharm El Sheikh nchini Misri ambapo kwa wiki ya kwanza viongozi wakuu wa nchi na Serikali wamekutana na kutoa hotuba zao.
Tanzania ni miongoni mwa nchi za Kiafrika zinazoshiriki mkutano huo ambapo Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan aliongoza ujumbe wa Tanzania na kutoa hotuba yake akielezea hatua za Serikali ya Tanzania katika kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Pia, Mhe. Rais Samia alipata wasaa wa kuzungumza katika moja ya Mikutano iliyoandaliwa na Benki ya Dunia kuhusu miradi mbalimbali ya mazingira inayosaidia kupunguza hewa ukaa.
Aidha, Ofisi ya Makamu wa Rais pamoja na taasisi zingine za Serikali na zisizo za kiserikali zinashiriki katika mkutano katika banda la maonesho la Tanzania ambalo wageni kutoka mataifa mbalimbali wanatembela na kupata elimu kuhusu Tanzania inavyofanya jitihada za kupambana na mabadiliko ya tabianchi.
Hotuba za viongozi hao zimejikita katika kuelezea changamoto zinazoikabili dunia kwa sasa ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa athari za mabadiliko ya tabianchi na kutoa mfano wa kuongezeka kwa ukame, joto kali, mafuriko, kupanda kwa kina cha bahari na kuyeyuka kwa barafu.
Wamesema athari za mabadiliko ya tabianchi ni dhahiri kwa sasa kwa kuwa kumekuwa na matukio kama vile dhoruba na vimbunga vimeendelea kuongezeka kwa siku za hivi karibuni kuliko hapo awali na inakadiriwa kuendelea kuongezeka.
Wakihutubia kwa nyakati tofauti katika mkutano huo, viongozi hao wamesisitiza na kuzitaka nchi zilizoendelea kuwajibika kwa kutoa rasilimali fedha, ufundi na teknolojia katika kusaidia nchi zinazoendelea kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuongezwa kwa fedha za kukabiliana na changamoto hiyo.
Kwa nyakati tofauti, viongozi hao wa nchi na Serikali wamesema kuwa katika mkutano huu wa COP27 ambayo inajulikana kama (COP ya Afrika) si muda wa kutoa ahadi bali ni kutoa utekelezaji wa ahadi kwa kuzingatia kaulimbiu ya mwaka huu ya COP27 isemayo "PAMOJA KWA UTEKELEZAJI".
Mkutano wa Viongozi wa Dunia umefanyika tarehe 7 na 8 Novemba, 2022 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Sharm El-Sheikh, Misri kwa ajili ya uzinduzi wa Mkutano wa Utekelezaji wa COP27. Zaidi ya Viongozi 100 wa Dunia walikusanyika kufanya kazi kuelekea utekelezaji wa makubaliano ya mabadiliko ya tabianchi.