Na Mwandishi wetu- Unguja
Katibu Mkuu Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) Bw. Islam Seif Salum amesema kuwa Wizara hiyo itaongeza kasi katika kuhakikisha urasimishaji biashara unakuwa chachu ya kuzalisha ajira visiwani humo baada ya Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Bishara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) kujenga uwezo ili kutekeleza azma ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwezesha wananchi kwa kuzalisha ajira zaidi katika sekta hiyo.
Ameyasema hayo leo katika eneo la Darajani Unguja wakati wa hafla ya uzinduzi wa Kituo jumuishi cha Biashara iliyoshirikisha wajumbe wa Kamati ya Uongozi ya MKURABITA waliopo ziarani visiwani humo kuwatembelea wanufaika wa mpango huo na kuona hatua walizofikia baada ya urasimishaji kufanyika kupitia mpango huo.
“Kituo hiki kinalenga kuwawezesha wananchi kupata huduma zote za urasimishaji biashara katika eneo moja ili kuwaondolea adha ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma katika Taasisi mbalimbali za Serikali, Wizara na Taasisi zilizopo chini yake zitaendelea kutenga bajeti ili kuwezesha suala la urasimishaji biashara kutekelezwa kwa kasi zaidi hali itakayochangia katika kuzalisha ajira kwa wingi zaidi na kukuza uchumi hapa Zanzibar”,alisisitiza Salum
Akifafanua amesema urasimishaji uliofanyika umeenda sambamba na kuwapatia mafunzo wafanyabiashara wadogowadogo ili waweze kusimamia biashara zao vizuri,kuweka kumbukumbu, kuwa na akaunti za biashara na kufanya biashara kwa tija.
“Katika hatua za ujenzi wa Kituo Wizara ilipokea kutoka MKURABITA jumla ya shilingi milioni 57,109,500/ambazo kati hizo shilingi milioni 27,969,000/- zilitumika katika shughuli za urasimishaji kwa Unguja na pemba na Shilingi milioni 29,140,500/ zilitumika kwa ajili ya ujenzi mdogo wa kuweka vibanda sita,ununuzi wa vifaambalimbali ikiwemo meza 6, viti6, kabati 1, Computer na vifaa vingine.
Kuhusu hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kuwezesha wananchi baada ya urasimishaji amesema kuwa ni pamoja na kupunguza ada ya usajili wa majina ya biashara,kuanzishwa kwa mfumo wa kielekrtoniki ili kusogeza zaidi huduma kwa wananchi.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Mpango huo Bi Immaculata Senje amesema kuwa kamati imeridhishwa na utekelezaji wa kazi za urasimishaji katika maeneo yaliyofikiwa na mpango huo visiwani humo.
Aidha, Bi. Senje amesema kuwa ushirikiano uliopo katika ya MKURABITA na Wizara hiyo umewezesha tija katika urasimishaji ardhi na biasahra Zanzibar.
Aliongeza kuwa kuna umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu urasimishaji biashara ili wajitokeze zaidi na kutumia fursa hiyo kuongeza tija.
Mratibu wa MKURABITA Dkt. Seraphia Mgembe amesema kuwa wananchi waliorasimisha biashara zao wameanza kuona faida ya mpango huo na azma ya mpango ni kuona idadi ya wanufaika inaongezeka zaidi ili kuendana na azma ya Serikali zote mbili.
Aliongeza kuwa mafanikio yaliyofikiwa ni chachu ya kuongeza kasi katika kuwahamasisha wananchi wengi zaidi kujitokeza na kurasimisha biashara zao ili ziweze kufanyika kwa kuzingatia mifumo ya sheria na taratibu zilizopo na pia kuwawezesha wananchi kunufaika na mikopo kutoka taasisi za fedha.
Akitoa taarifa ya urasimishaji visiwani humo , Mkurugenzi wa Biashara na Masoko Bw. Khamis Ahmada Shauri amesema kuwa jumla ya wafanyabiashara 461 wamerasimisha biashara zao visiwani humo baada ya kujengewe uwezo kupitia mafunzo yaliyoendeshwa na MKURABITA na Wizara hiyo katika awamu zote za urasimishaji hadi kufikia mwaka 2020.
MKURABITA na Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), pamoja na Tume ya Mipango imefanikiwa katika kuwezesha wananchi kurasimisha biashara na ardhi ili kujikwamua kiuchumi na kushiriki katika ujenzi wa uchumi.
Mmoja wa wanufaika wa urasimishaji biashara uliofanywa na MKURABITA kwa kushirikiana na Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) Bi. Mariam Abdalla Hemed akieleza faida alizopata baada ya kurasimisha biashara yake ikiwemo kukopa fedha za kukuza biashara yake.
Sehemu ya bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali walirasimisha biashara zao katika Wilaya mbalimbali ikiwemo wilaya ya Magharibi B, Unguja Zanzibar.
(Picha na MAELEZO)