Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mkirikiti: Epukeni Kuishi Maeneo Yasiyo na Anwani za Makazi
Mar 02, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na. OMM Rukwa

Serikali imeshauriwa kutoa elimu kwa wananchi hususan wanaoishi kwenye maeneo ya vyanzo vya maji na mabondeni endapo wanastahili kupatiwa anwani za makazi na postikodi.

Ushauri huo umetolewa na mwakilishi wa Shirika la Sumango, Vincent Kuligi wakati akichangia mada ihusuyo umuhimu wa zoezi la utambuzi makazi na uwekaji posticodi kwenye kikao cha Kamati ya Ushauri Mkoa wa Rukwa kilichofanyika jana mjini Sumbawanga.

“Kuna watu wamejenga katika vyanzo vya maji. Je watahamishwa kabla ya kupata anwani za makazi au watapewa namba za nyumba huko huko wakati wa zoezi hili hapa kwetu Sumbawanga?” alihoji mwananchi huyo Vincent.

Akitoa ufafanuzi wa hoja hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joseph Mkirikiti alisema lengo la Serikali ni kutambua uhai wa watu wake ikiwemo kujua mahala gani wanaishi hivyo utambuzi wa makazi yao utafanyika licha ya kuwa wanaishi mabondeni.

Mkirikiti aliongeza kusema wataalam wa utambuzi wa anwani za makazi watafika maeneo yote ambako watu wanaishi na kuwaingiza kwenye regista ikiwemo nyumba zao ambapo alitoa wito kwa taasisi za TANROAD, TARURA na Shirika la Posta kushirikiana na Halmashauri katika zoezi hilo.

“Kwa walio mabondeni na maeneo yaliyozuiwa tutawahesabu huko huko kisha kuwaeleza endapo wanaostahili au la kuishi maeneo hayo kwa mujibu wa sheria za nchi”, alisema Mkirikiti.

Mkuu huyo alisisitiza na kutoa wito kwa viongozi wa vitongoji, vijiji, kata na wilaya kuwaelimisha wananchi juu ya kushiriki kwenye zoezi la utambuzi wa makazi na uwekaji anwani ili maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwezi Agosti mwaka huu ifanikiwe.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa, Jonas Kilima Akiwasilisha mada juu ya maandalizi ya utekelezaji wa mfumo wa uwekaji anwani za makazi na postikodi alisema Halmashauri zote nne zimeanza kutekeleza maelekezo ya serikali.

Aidha, Kilima alisema uhamasishaji jamii kuhusu zoezi hilo ikiwemo utambuzi wa majina ya barabara na mitaa pamoja na makazi imeanza katika Halmashauri za Manispaa ya Sumbawanga, Sumbawanga DC, Nkasi DC na Kalambo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi