Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mkandarasi Jengo la Wizara ya Nishati Atakiwa Kukamilisha Kazi ya Ujenzi kwa Wakati
Dec 28, 2018
Na Msemaji Mkuu

                        Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani

 Na; Mwandishi Wetu- Dodoma

Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani amemtaka mkandarasi anayetekeleza kazi ya ujenzi wa Jengo la Wizara ya Nishati  linalojengwa katika Mji wa Serikali,  Ihumwa jijini Dodoma kuhakikisha kuwa anakamilisha kazi hiyo kwa wakati uliopangwa.

Akizungumza katika eneo la Ihumwa  Waziri Kalemani  amesema kuwa, ili kufanikisha utekelezaji wa kazi hiyo kwa wakati ni vyema mkandarasi huyo ambaye ni Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) akahakikisha kuwa  vifaa vyote vinavyotakiwa katika kutekeleza kazi hiyo vinakuwepo katika eneo la kazi.

"Ni Lazima mkandarasi  uhakikishe kuwa matofali, mchanga, simenti, mabati, kokoto, rangi, madirisha, nondo na vifaa vyote vinavyotakiwa hapa kwa ajili ya ujenzi vinapatikana  kwa wakati wote katika eneo hili la ujenzi ili kuharakisha utekelezaji wa kazi hii kama ulivyopangwa na si vinginevyo";

Akifafanua,  Dkt. Kalemani amesema kuwa atakuwa akitembelea eneo hilo mara kwa mara kuona hatua za utekelezaji wa kazi hiyo na kuwaasa watendaji wa Wizara yake kuhakikisha kuwa wanafuatilia kwa karibu kazi husika ili itekelezwe kwa viwango vinavyotakiwa na kwa wakati.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Hamisi Mwinyimvua amemtaka mkandarasi huyo kuhakikisha kuwa anaongeza mitambo inayotakiwa katika kutekeleza ujenzi huo ili kuongeza kasi ya utekelezaji.

Ujenzi wa jengo la Wizara ya Nishati ni utekelezaji wa Agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa Wizara zote kujenga majengo katika eneo hilo la Ihumwa unakojengwa mji wa Serikali unaojumuisha majengo ya Wizara zote.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi