[caption id="attachment_39263" align="aligncenter" width="900"] Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (mbele) akiwa amefuatana na Katibu Mkuu, Dkt Hamisi Mwinyimvua pamoja na viongozi mbalimbali wa Wizara; kukagua maendeleo ya ujenzi wa ofisi ya wizara katika mji wa serikali, Ihumwa. Ziara hiyo ilifanyika Desemba 28, 2018.[/caption]
Na Veronica Simba – Dodoma
Imeelezwa kuwa eneo la Ihumwa, kunakojengwa ofisi za wizara na taasisi za serikali, litatandazwa mfumo wa njia ya umeme chini ya ardhi badala ya uliozoeleka wenye nguzo zilizosimikwa juu ya ardhi, ili kulipendezesha.
Hayo yalibainika jana, (Desemba 28, 2018) wakati Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani alipotembelea eneo hilo na kukagua shughuli za ujenzi wa ofisi ya wizara ya nishati pamoja na maeneo kunakopita miundombinu ya umeme.
Akitoa maelezo kuhusu mpango wa upelekaji umeme katika eneo hilo, Kamishna wa Umeme na Nishati Mbadala, Mhandisi Innocent Luoga, alimweleza Waziri Kalemani ambaye alifuatana na Katibu Mkuu Dkt Hamisi Mwinyimvua, kuwa mbali na kuupendezesha mji huo wa serikali, pia mfumo wa umeme unaopita chini ya ardhi utasaidia upatikanaji wa nishati hiyo muhimu kwa uhakika.
[caption id="attachment_39264" align="aligncenter" width="819"] Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (mwenye suti ya bluu) akijadiliana jambo na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Josephat Kakunda (kushoto); walipokutana Ihumwa, wakati wakikagua maendeleo ya ujenzi wa ofisi za wizara zao, Desemba 28, 2018. Kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt Hamisi Mwinyimvua.[/caption]“Unapokuwa na mfumo wa umeme unaopita chini ya ardhi, unakuwa na umeme wa uhakika na pia matengenezo mbalimbali kama vile kurekebisha nyaya zilizokatika yanapungua sana maana hauathiriwi sana kwa kuwa umefunikwa,” alifafanua.
Pia, Kamishna Luoga aliongeza kuwa, mfumo huo utaondoa kwa kiasi kikubwa tatizo la ukatikaji umeme.
Hata hivyo, alibainisha kuwa, mpango wa kutandaza mfumo huo ni wa muda mrefu ambao utaanza kutekelezwa siku za usoni na kwamba kwa sasa unatekelezwa mpango wa muda mfupi, unaohusisha kusambaza umeme eneo hilo kwa njia ya kawaida inayotumia nguzo zinazosimikwa juu ya ardhi.
Akieleza zaidi, Luoga alisema lengo la kuanza na mpango huo wa muda mfupi ni ili kusaidia kufanya kazi za awali, ambapo kufikia mwishoni mwa Januari mwakani, ofisi zote mahali hapo ziwe na umeme.
[caption id="attachment_39265" align="aligncenter" width="900"] Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (wa pili-kushoto), akitoa maelekezo kwa Kaimu Meneja wa TANESCO Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Tumaini Nyale (kulia), wakati wa ziara aliyoifanya Desemba 28, 2018 kukagua maendeleo ya ujenzi wa ofisi ya wizara na shughuli za upelekaji miundombinu ya umeme katika mji wa Serikali Ihumwa.[/caption]Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Tumaini Nyale, alimweleza Waziri na Katibu Mkuu kuwa, ofisi yake imejipanga kikamilifu kuhakikisha eneo hilo linasambaziwa umeme kwa kasi. “Vifaa vyote vipo na kila mteja atakayelipia ataunganishiwa umeme mara moja.”
Waziri Kalemani, alitumia fursa hiyo kuwahamasisha viongozi wa wizara na taasisi zote zinazojenga ofisi zao Ihumwa, kulipia gharama za kuunganishiwa umeme, ili wapatiwe huduma hiyo muhimu na hivyo kuendelea na utekelezaji wa shughuli mbalimbali kwa ufanisi.
Alizipongeza wizara ambazo zimekwisha kuchukua fomu za maombi ya kuunganishiwa umeme, ambazo alizitaja kuwa ni Maji, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera), Elimu na Nishati yenyewe.
Awali, akizungumza na mkandarasi anayejenga ofisi za wizara ambaye ni Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Waziri Kalemani alimtaka kuongeza kasi na kuhakikisha analeta vitendea kazi vyote eneo hilo, pamoja na kuongeza idadi ya vibarua ili akamalishe jengo hilo na kulikabidhi kwa wizara mwishoni mwa Januari mwakani kama yalivyo makubaliano.
Katika ziara hiyo, Kamati ya Wizara inayosimamia shughuli za ujenzi wa ofisi husika, ikiongozwa na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Raphael Nombo, ilishiriki pia.
[caption id="attachment_39262" align="aligncenter" width="900"] Njia ya umeme wa kilovolti 33 na urefu wa kilomita 14.6 inayopeleka umeme katika mji wa serikali wa Ihumwa, Dodoma. Taswira hii ilichukuliwa Desemba 28, 2018 wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani kukagua maendeleo yaujenzi wa ofisi ya wizara na shughuli za upelekaji miundombinu ya umeme katika eneo husika.[/caption](Picha na Wizara ya Nishati)