[caption id="attachment_40961" align="aligncenter" width="927"] Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akizungumza wakati wa hafla ya uwashaji rasmi wa umeme katika kijiji cha Ntauna, Kata ya Rondo, Lindi Vijijini, akiwa katika ziara ya kazi, Februari 27, 2019.[/caption]
Na Veronica Simba – Lindi
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amewataka watanzania kuondoa shaka kuhusu mipango ya serikali kufuatia gesi iliyogunduliwa mikoa ya kusini, kwani haijabadilika na inaendelea kutekelezwa.
Aliyasema hayo jana Februari 27, 2019 kijijini Ntauna, Kata ya Rondo, Lindi Vijijini, alipokuwa akihitimisha ziara yake ya siku nne mkoani Lindi ambapo alikagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme, kuwasha umeme katika vijiji mbalimbali na kuzungumza na wananchi.
“Nataka niwaaminishe wana-kusini, yale ambayo serikali iliahidi baada ya kugundua gesi, mipango yake iko palepale na inafanyiwa kazi,” alisema.
Akifafanua zaidi, Naibu Waziri Mgalu alisema moja ya mambo ambayo serikali iliahidi ni umeme wa uhakika utakaowezesha uwekezaji. Alisema hadi sasa, taratibu za kukamilisha ujenzi wa Mradi wa kuzalisha umeme wa gesi Mtwara wenye megawati 300 na Somanga Fungu wenye megawati 330 ziko katika hatua za mwisho.
[caption id="attachment_40962" align="aligncenter" width="750"] Sehemu ya umati wa wananchi wa kijiji cha Mvuleni, Lindi Vijijini, wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao kabla ya kuwasha rasmi umeme kijijini hapo, Februari 27, 2019.[/caption]“Mradi utaanza ndani ya mwaka huu wa fedha ambao utawezesha mikoa hii kuzalisha umeme wa kutosha kuweza kuingizwa kwenye Gridi ya Taifa.”
Aidha, aliongeza kuwa, jambo jingine kubwa ni kuviwezesha viwanda vya maeneo husika kupata umeme wa gesi ambapo alisema tayari kiwanda cha saruji cha Dangote kimeshaunganishiwa.
Pia, alisema, serikali inaendelea kuzungumza na viwanda vya mbolea ili vizalishe mbolea inayotokana na gesi ili pamoja na mambo mengine viongeze ajira kwa wananchi.
Vilevile, alisema kwa Mkoa wa Lindi, eneo la Likongo, serikali inatarajia kujenga kiwanda cha kusindika gesi iwe katika hali ya kimiminika ambapo Rais John Magufuli ametoa mwongozo wa kufanya mazungumzo na mbia mmoja mmoja. Alisema mazungumzo yanaendelea vizuri.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri alizungumzia tathmini ya ziara yake mkoani Lindi, ambapo alisema imekuwa yenye mafanikio.
alisema, kazi ya kuwaunganishia wananchi umeme vijijini inaendelea na ametoa wito kwa mkandarasi husika kuboresha utendaji wake ili kuhakikisha anafikia malengo ya kukamilisha kazi yote kwa mujibu wa mkataba ifikapo Juni 30, mwaka huu ambapo ndipo mradi wa umeme vijijini awamu ya tatu, mzunguko wa kwanza utakuwa unahitimishwa.
Naibu Waziri alisema yeyé pamoja na viongozi wengine wa Lindi akiwemo Mkuu wa Mkoa, Wakuu wa Wilaya na Wabunge wamekubaliana kumsimamia mkandarasi husika katika kuhakikisha anatimiza wajibu wake ipasavyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga, ambaye alifuatana na Waziri wakati akihitimisha ziara yake, aliwahakikishia wananchi wa eneo husika kuwa yeyé pamoja na viongozi wenzake watamsimamia mkandarasi husika ili kuhakikisha kazi inatekelezwa kwa ufanisi.
“Tumekabidhiwa hawa tuwasimamie, kwa hiyo nichukue nafasi hii kuwathibitishia kwamba tutawasimamia kwelikweli ili kuhakikisha zoezi hili linakamilika vizuri sana,” alisisitiza.
Naye Mbunge wa Jimbo la Mtama, Nape Nnauye, aliipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa upande wa nishati ambapo alisema imekuwa ikifanya kazi nzuri sana.
“Tunawashukuru sana Wizara ya Nishati kwa kazi nzuri wanayoifanya. Kama kuna Wizara inafanya vizuri, basi Wizara hii inafanya vizuri.”
[caption id="attachment_40963" align="aligncenter" width="750"] Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (kulia) akiwasha rasmi umeme katika kijiji cha Ntauna, Kata ya Rondo, Lindi Vijijini, akiwa katika ziara ya kazi, Februari 27, 2019. Wengine pichani ni Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga (kushoto), Mbunge wa Jimbo la Mtama, Nape Nnauye (wa pili-kushoto) na Afisa wa TANESCO Lindi.[/caption]Hata hivyo, Nnape alisema anatambua kiu kubwa ya umeme waliyonayo wananchi na kuwasihi kuwa wastahimilivu maana zoezi la kuunganisha umeme ni hatua kwa hatua, awamu kwa awamu. Alisema anayo imani kubwa kwamba vijiji vyote vitafikiwa na huduma hiyo kabla ya mradi kuisha.
Mkuregenzi wa kampuni ya State Grid, ambayo ndiyo inatekeleza uunganishaji wau meme mkoani Lindi, Charles Mlawa, akizungumza na waandishi wa habari baada ya ziara hiyo, aliahidi kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na Naibu Waziri katika kuhakikisha kazi hiyo inafanyika kwa ufanisi.
Katika ziara hiyo, viongozi wa ngazi mbalimbali walipongeza utendaji kazi wa Wizara pamoja na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na kuomba jitihada zinazofanyika ziendelee.
Katika Miradi ya Umeme Vijijini, Mzunguko wa Kwanza (REA III – 1), jumla ya vijiji takribani 133 vitaunganishiwa umeme kwa gharama ya shilingi bilioni 31.9. Matarajio ni kuwaunganishia wananchi takribani 5337.
Akiwa Lindi vijijini, Naibu Waziri aliwasha umeme katika vijiji vya Ntauna, Mvuleni na Tulieni.