Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Milioni 806 Zatumika Kujenga Miundombinu ya Sekondari Mtwango
Jan 09, 2024
Milioni 806 Zatumika Kujenga Miundombinu ya Sekondari Mtwango
Muonekano wa madarasa ya kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari Mtwango yaliyojengwa na Serikali yaliyopo katika Kata ya Mtwango, Halmashauri ya Wilaya ya Njombe mkoani Njombe.
Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO

Jumla ya shilingi milioni 806 zilizotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita katika mwaka wa fedha 2022/23, zimetumika kujenga miundombinu ya kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari Mtwango iliyopo katika Kata ya Mtwango, Halmashauri ya Wilaya ya Njombe mkoani Njombe.

Akizungumza hivi karibuni na Maafisa Habari kutoka Idara ya Habari-Maelezo, Kaimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Mtwango, Julius Stambuli amesema kuwa fedha hizo zilitolewa kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 10 ambapo tayari madarasa 7 yamekamilika na mengine yapo katika hatua mbalimbali, ujenzi wa mabweni 4 ambapo moja limekamilika na matatu yapo katika hatua za umaliziaji na matundu ya vyoo 18 ambapo matundu 16 yamekamilika na mawili yapo katika hatua za umaliziaji.

"Shule hii ilikuwa na changamoto za uchakavu na uhaba wa miundombinu, tunaishukuru serikali kwanza ilileta shilingi milioni 300 kwa ajili ya ukarabati wa madarasa matano na ofisi za Walimu na kwa sasa imetuletea milioni 806 ambazo tunaendelea na ujenzi wa miundombinu mingine. Kuimarika kwa miundombinu kumeongeza idadi ya wanafunzi kufikia wanafunzi 898," alisema Mwalimu Stambuli.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Mtwango, Rhoida Wanderage ameipongeza serikali kwa kuendelea kuwajali wananchi wa Mtwango ambapo kwa mwaka wa fedha 2022/23, imewaletea shilingi bilioni 1.9 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa Kituo cha Afya, Zahanati na Shule.

“Pamoja na ukarabati wa shule hii, tunashukuru pia kwa kuletewa Walimu wa kutosha kwani shule ilikuwa na Walimu 8 lakini kwa sasa ina Walimu 39, kutokana na ubora wa miundombinu hii, Walimu wana ari ya kufundisha na wanafunzi wanafundishwa katika mazingira bora," amesema Bibi Rhoida.

Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzie, Dominick Kifaru amesema kuwa kabla ya ujenzi wa madarasa hayo kulikuwa na msongamano wa wanafunzi madarasani lakini kwa sasa wanakaa madarasa yenye nafasi na ubora hali itayopelekea wanafunzi kusoma kwa bidii. Pia, ameishukuru Serikali kwa kuwajengea mabweni.

Shule hiyo ilianzishwa mnamo mwaka 1958 ikiwa ni "Middle School", mwaka 1983 ilisajiliwa kutoa elimu ya sekondari chini ya Shirika la Maendeleo ya Wilaya Njombe (NDDT) ambalo kutokana na changamoto mbalimbali baadaye walishindwa kuiendeleza. Tangu mwaka 2021, shule hiyo ilianza kumilikiwa na Serikali.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi