Jumla ya shilingi milioni 67 imetolewa na Serikali ya Awamu ya Sita kwa ajili ya mikopo ya vijana, wanawake na wenye ulemavu katika Kata ya Lukarasi, iliyopo Mbinga Vijijini mkoani Songea.
Afisa Maendeleo wa Jamii wa Kata hiyo, Bi. Deodata Mbunda amesema hayo wakati wa mahojiano maalum na Maafisa wa Idara ya Habari-MAELEZO walipotembelea wilayani hapo mwishoni mwa mwezi Desemba, 2024.
“Mpaka sasa Serikali ya Mama Samia imetupatia Kata ya Lukarasi shilingi milioni 67, katika vijiji vitatu, Kijiji cha Mpiringa, Lukarasi na Kijiji cha Liula, kupitia makundi ambayo yalikuwa yamesahaulika, ambavyo ni vikundi vya wakina mama, watu wenye ulemavu pamoja na vijana,” amesema Bi. Deodata.
Ameendelea kusema kuwa, baadhi ya vikundi huwa wanafanya biashara za ujasiriamali, ikiwemo utengenezaji wa batiki, ufugaji wa nguruwe, kuku pamoja na mbuzi. Makundi mengine yana mabwawa ya samaki na wengine wanafanya kilimo.
Aidha amesema kuwa, vikundi hivyo vimekuwa vikifanya vizuri katika biashara zao, hivyo kurejesha kwa wakati mikopo walioichukua, na mara wanapomaliza marejesho ya mikopo hiyo huomba tena mikopo mingine kwa ajili ya kukuza zaidi biashara zao.
Akitolea mfano Kikundi cha Amani Vikoba kinachojihusisha na ukamuaji wa Mafuta ya Alizeti na Ufugaji, Bi Deodata amesema, “Kikundi cha Amani Vikoba kilipewa mkopo wa shilingi milioni 4 mwaka 2019. Wakarejesha kwa haraka sana, wakaomba tena mkopo mwingine wa shilingi milioni 27 ambayo imewasaidia kujenga kiwanda kidogo cha kukamulia mafuta ya alizeti pamoja na mashine za kisasa za kukamulia”.
Amesema mradi wa Amani Vikoba umesaidia kutoa ajira kwa vijana, vilevile wakulima wa Alizeti wamekuwa na uhakika wa sehemu ya kuuza mazao yao.
Naye Mwenyekiti wa Kikundi cha Amani Vikoba, Bi. Anna Ndimbo ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kupata mikopo ya asilimia kumi. Amesema walikuwa wakipata shida sehemu ya kwenda kukamulia Alizeti, ambapo walikuwa wakisafiri mpaka wilaya nyingine kwa ajili ya kufuata huduma hiyo.
“Mkopo wa asilimia 10 umetuwezesha kupata mashine ya kuchakata na kuchuja mafuta ya Alizeti. Hivyo tumenufaika kwa asilimia 95 kwa uwepo wa mashine hizo, kwani tunachakata alizeti zetu hapahapa kijijini, hatutumii fedha yoyote kwa ajili ya nauli, wala usafirishaji wa Alizeti.” Amesema Bi. Anna.