Mikoa ya Kanda ya Kaskazini imehakikishiwa kupata umeme wa uhakika utakaowasaidia kuondokana na adha ya kukatika kwa umeme mara kwa mara.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa uhakika huo kwa wananchi wa kanda hiyo leo Machi 9, 2025, wakati akizindua mradi wa maji wa Mwanga-Same-Korogwe uliopo Wilaya ya Mwanga, mkoa wa Kilimanjaro.
Rais Samia amebainisha kuwa, Serikali iko katika hatua za mwisho kukamilisha utaratibu wa kununua umeme kutoka nchi jirani kwa ajili ya mikoa ya Kaskazini inayojumuisha Kilimanjaro, Tanga, Arusha na Manyara.
Amesema dhamira ya Serikali yake ni kuhakikisha wananchi wote wanafikiwa na huduma ya maji, umeme na huduma zote muhimu kwa ustawi wao.
Rais Samia amezindua mradi wa maji wa Same-Mwanga-Korogwe utakaonufaisha wakazi wa wilaya hizo zaidi ya laki nne.