Inaelezwa kuwa chimbuko la uhusiano kati ya Tanzania na Indonesia ni Mkutano wa Bandung uliofanyika mwaka 1955 ambapo nchi nyingi za Afrika na Asia zilikuwa katika utawala wa kikoloni kwa kipindi hicho.
Kupitia Mkutano huo nchi hizo zilikubaliana kuimarisha ushirikiano ili kujikomboa kutoka katika utawala wa kikoloni na ulikuwa ndiyo msingi wa kuanzishwa kwa Umoja wa Nchi zisizofungamana na Upande Wowote (Non- Aligned Movement –NAM).
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax, leo jijini Dar es salaam wakati wa mkutano na Wahariri na Waandishi wa Habari, amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Indonesia, Mhe. Joko Widodo atawasili nchini leo tarehe 21 Agosti, 2023 na atapokelewa rasmi na mwenyeji wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, tarehe 22 Agosti, 2023, Ikulu jijini humo.
Aidha, Mhe. Dkt. Tax amesema kuwa mwaka 2024 Tanzania na Indonesia zinatimiza miaka 60 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia ikiwa ni pamoja na kushirikiana katika harakati za ukombozi na kuwa uhusiano huo umekuwa na mafanikio makubwa.
“Hadi kufikia mwaka 2023, Indonesia imewekeza nchini miradi ipatayo mitano katika sekta mbalimbali ikwemo za kilimo, uzalishaji wa viwandani na ujenzi. Mwaka 1996 Indonesia ilianzisha Kituo cha Mafunzo ya Kilimo kwa Wakulima Vijijini kilichopo Mikindo mkoani Morogoro. Kituo hicho kimekuwa kikitoa mafunzo mbalimbali kwa wakulima”, ameeleza Dkt. Tax.
Pia, amefafanua “Kwa kuzingatia kuwa, Indonesia imepiga hatua kubwa katika kilimo cha zao za chikichi kutokana na kuwa na mbegu bora ya zao hilo, pamoja na teknolojia ya kisasa, ziara ya Mhe. Rais Widodo nchini itapanua wigo wa ushirikiano katika zao la chikichi utakaowawezesha wakulima wetu wa zao hilo kunufaika na mbegu bora ya chikichi, na hivyo kuwajengea uwezo na kuongeza uzalishaji wa mafuta ya kula”.
Miongoni mwa masuala yanayotarajiwa katika ziara hiyo ni kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali kama itakavyoonekana katika hati za makubaliano zitakazosainiwa na matokeo ya mazungumzo baina ya viongozi wa mataifa hayo mawili yatakayojikita katika diplomasia, biashara, kilimo, uvuvi, elimu, nishati, madini, uchumi wa buluu na uhamiaji.