Na Ahmed Sagaff – MAELEZO
Siku ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar inatarajiwa kuadhimishwa kipekee tofauti na ilivyokuwa ikisherehekewamiaka iliyopita.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano naMazingira), Mhe. Selemani Jafo amesema kwamba Aprili 26, 2022 Serikali itazindua andiko linaloelezea historia, misingi na maendeleo ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambalo litatumika kuelimisha umma.
“Baada ya uzinduzi, Ofisi ya Makamu wa Rais imepanga kuwa na mpango endelevu wa kutoa elimu kwa umma kuhusu historia ya Muungano na masuala ya msingi kuhusu Muungano, inatarajiwa kuwa mpango wa elimu kwa umma utaongeza uelewa wa historia ya Muungano na masuala mengine muhimu kuhusu Muungano,” ameeleza Mhe Jafo.
Pamoja na uzinduzi wa andiko hilo, Serikali imeandaa kongamano la miaka 58 ya Muungano litakaloendeshwa kwa umahiri na wabobezi wa mambo ya Muungano ambao wataeleza kwa kina historia ya Muungano, misingi ya Muungano na mafanikio ya Muungano.
“Maadhimisho ya miaka 58 ya Muungano yatarushwa mubashara na Vyombo vya Habari ikiwemo luninga, redio na mitandao ya kijamii ya Tanzania Bara na Zanzibar,”amehabarisha Waziri Jafo.
Sambamba na hayo, Serikali imeandaa mashindano ya insha kuhusu Muungano kwa wanafunzi wa shule za sekondari ambapo kutakuwa na washindi sita ambapo watatu watatoka Tanzania Bara na waliobakia watatoka Zanzibar ambao watapatiwa zawadi siku ya kilele cha maadhimisho.
“Insha hizo zinawapa fursa wanafunzi kuelezea historia yaMuungano, mafanikio na changamoto za Muungano, na nafasi ya vijana katika kulinda na kudumisha Muungano,” amebainisha waziri huyo.
Mnamo Aprili 26, 1964 Rais wa Tanganyika, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Rais wa Zanzibar, Mzee Abeid Amaan Karume waliunganisha himaya mbili na kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambayo baadae iliitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.