Na: Ramadhani Kissimba na Josephine Majura - WFM DAR ES SALAAM
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba amewataka Wanamipango nchini kuwa makini, katika kupanga mipango ambayo wataweza kuitekeleza, kuifuatilia na kuitolea taarifa sahihi.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango katika ufunguzi wa kongamano la Wanamipango Jijini Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Lawrence Mafuru aliwataka Wanamipango hao kujikita zaidi katika kuleta mabadiliko chanya ya kiuchumi na kijamii ili kuleta maendeleo katika sekta mbalimbali.
Bw. Mafuru amewataka wanamipango hao kuendelea kuishauri Serikali njia bora ya kusimamia kikamilifu mipango ya nchi ili kufikia maendeleo au mafanikio ya uchumi wa kipato cha juu kinachokusudiwa.
"Nawasihi wote kwa umoja wenu kuwa na mchango na ushauri wenye lengo la kupanga na kusimamia kikamilifu mipango ya nchi yetu. Uwezo wenu madhubuti utaisaidia Serikali na Nchi kwa ujumla kuwa na mipango imara na njia sahihi ya kufikia maendeleo au mafanikio ya uchumi wa kipato cha juu tunaoutamani", alisema Bw. Mafuru
Aidha, alifafanua kuwa kwa kuzingatia umuhimu wa Wanamipango, Serikali ya Awamu ya Sita imeweka msukumo wa kipekee wa kuimarisha kada ya Wanamipango ili Taifa liweze kupanga mipango shirikishi inayotekelezeka kwa maendeleo ya watu wake si kwa kizazi cha sasa pekee bali na kizazi kijacho.
Awali akiongea wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo, Kamishina wa Idara ya Mipango ya Kitaifa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Mursali Milanzi alisema wanamipango ndio wanaondaa, kusimamia, kutekeleza na kufanya ufuatiliaji na tathmini ya mipango ya nchi.
Bw. Milanzi alisema kongamano la wanamipango hufanyika kila mwaka kwa lengo la kubadilishana uwezo na mada mbalimbali zitakazowasilishwa, kubwa zaidi kongamano hilo litatumika katika kujadili kuhusu Dira mpya ya Maendeleo ya Taifa, ambapo Dira inayoisha 2025 ilikuwa na dhima ya kuipeleka nchi kwenye uchumi wa kati ambapo nchi ilifikia lengo hilo miaka mitano kabla ya Dira hiyo kuisha, hivyo kongamano hili litatumika kuyalinda mafanikio yaliyopatikana katika Dira ya Maendeleo 2025 kwa kuja na Dira mpya ambayo itakuwa na mafanikio kuliko Dira tuliyonayo saa.
Bw. Mafuru aliwakumbusha Wanamipango chini ya mlezi wa wanamipango nchini ambaye ni Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango kuhusu jukumu lao la msingi la kusimamia kikamilifu ufuatiliaji wa Mipango ya nchi ili kuhakikisha rasilimali za nchi zinatumika kama ilivyopangwa.
"Labda niwakumbushe tu kuwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mara kadhaa amesema kuhusu UDHAIFU WA KUFUATILIA MIPANGO YETU, suala hili kimsingi linaangukia kwenu Wanamipango. Nawaasa, chini ya Mlezi wenu kuwa makini katika kupanga mipango ambayo mtaweza kuitekeleza, kuifuatilia na kuitolea taarifa pasipo na shaka yoyote", aliongeza Bw. Mafuru.
Aidha, Bw. Mafuru alisema kuwa kongamano hilo limekuja katika muda muafaka ambapo maandalizi ya awali ya Dira mpya ya Taifa ya Maendeleo 2050 (TDV 2050) yameanza kutokana na nchi kuwa katika hatua za mwisho za utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 kupitia Mpango wa Tatu wa Miaka Mitano wa Maendeleo wa Taifa 2020/21 - 2025/26., hivyo kuwataka wanamipango kutumia kongamano hilo kuwa sehemu ya maandalizi ya Dira shirikishi ambayo itajumuisha maoni ya wadau wote muhimu.
Kongamano la mwaka la wanamipango linafanyika kwa siku tatu kuanzia tarehe 5 Desemba, 2022 lilobeba dhima ya ‘Mageuzi ya kiuchumi na kijamii kwa kizazi kijacho’ na limeshirikisha wachumi, wanamipango na watakwimu kutoka Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Taasisi na Mashirika ya Umma, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.