Waziri wa Afya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Nassor Ahmed Mazrui ameipongeza Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushiriki maonesho ya wiki ya afya Zanzibar na kutoa elimu ya namna ya kujikinga na magonjwa ya moyo pamoja na kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa hayo kwa wakazi wa Zanzibar.
Waziri Mazru ametoa pongezi hizo alipotembelea banda la JKCI katika maonesho ya Wiki ya Afya Zanzibar yanayofanyika katika Hoteli ya Golden Tulip Airport.
“Nawapongeza JKCI kwa kuwafikishia wakazi wa Zanzibar elimu na huduma hizi muhimu za matibabu ya moyo, mmekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kila mwananchi anafikiwa na huduma hizi,” alisema Mhe. Mazrui.
Mhe. Mazrui ameitaka JKCI kuendelea kuwahudumia wakazi wa Zanzibar bila kuchoka kwani wakazi hao wanawahitaji.
Aidha, Mhe. Mazrui ameipongeza Taasisi isiyo ya kiserikali ya Heart Team Africa Foundation (HTAF) kwa kutumia maonesho hayo kutafuta fedha za kusaidia upasuaji wa moyo kwa watoto wanaotibiwa JKCI.