Na Shamimu Nyaki
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe.Pauline Gekul amesisitiza jamii kutekeleza maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mhe. Samia Suluhu Hassan ya kufanya mazoezi kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi.
Mhe. Gekul amesema hayo wakati alipokua Mgeni Rasmi kwenye mashindano ya mbio mjini Moshi ya Mr UK Marathon yaliyofanyika wilayani hapo Desemba 11, 2022 mkoani Kilimanjaro na kusisitiza kuwa mazoezi yanaimarisha afya, yanajenga uhusiano na upendo.
"Nawasisitiza Wananchi kuendelea kutekeleza agizo la Mhe. Rais Samia la kufanya mazoezi ili kuimarisha afya zetu na kujikinga na maradhi yasioambukiza, ili tuwe na afya njema tuweze kufanya shughuli za kuongeza kipato cha Jamii na Taifa letu", amesisitiza Mhe. Gekul.
Mhe. Gekul amewaasa Wandaaji wa Marathon mbalimbali na mabonanza nchini kushirikisha wazee, walemavu, na watoto ili nao washiriki kama ilivyo kwa vijana kwa sasa.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Moshi Mjini, Mhe. Abbasi Kayanda amesema marathon hiyo imesaidia Wananchi wa Moshi kuhamasika kufanya mazoezi pia imeinua uchumi wao na kutoa wito kwa wadau wengine kujitokeza kufanya mabonanza mengine ya michezo.
Marathon hiyo imeshirikisha mbio za KM 10, 5 na 2 kwa wanaume na wanawake ambapo washindi wamepatiwa Medali na zawadi mbalimbali