Na Shamimu Nyaki – WUSM, Dodoma
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Pauline Gekul ameuagiza uongozi wa Chama Cha Netiboli nchini (CHANETA) ufike katika Mikoa na Halmashauri zote nchini ili kuibua vipaji vya mchezo huo.
Naibu Waziri Gekul ametoa agizo hilo leo Mei 20, 2022 jijini Dodoma alipokutana na kufanya mazungumzo na uongozi mpya uliofika kujitambulisha kwa Naibu Waziri baada ya kufanya uchaguzi kwa ukamilifu.
"Hongereni sana wa kufanya uchaguzi, Wizara tupo tayari kushirikiana na nyie katika kuendeleza netiboli nchini, na nawaahidi wizara itakutana na nyie kuona mpango mkakati wenu wa kuendeleza mchezo huu," alisema Naibu Waziri Gekul.
Mhe. Gekul amewaagiza viongozi hao kutatua changamoto zote zinazokabili mchezo huo ambao kwa sasa haufanyi vizuri na kuwataka kuyatumia mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA kupata wachezaji wazuri watakaoliwakilisha vyema Taifa.
Kwa upande wake, Katibu wa chama hicho, Rose Mkisi alieleza kuwa Chama hicho kimepata uongozi bora ambao unazingatia miiko, uwazi, uwajibikaji na katiba katika kuongoza na kukuza mchezo wa netiboli nchini.
Uongozi wa chama hicho utadumu kwa muda wa miaka minne na imeainisha vipaumbele vyake ikiwemo kuibua vipaji na kuviendeleza pamoja na uandaaji, usimamizi na uratibu wa mashindano katika ngazi mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.