Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mgombea Mmoja wa Udiwani Aenguliwa, Saba Wanusurika
Aug 30, 2018
Na Msemaji Mkuu

Idara ya Habari-NEC

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imefanya uamuzi wa rufaa nane za wagombea udiwani wa kata saba zinazoshiriki uchaguzi mdogo na kukubali rufaa ya kumuengua mgombea mmoja wa kata ya Sisimba  katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya.

Akitoa taarifa ya uamuzi wa rufaa hizo jijini Dar es Salaam leo (Agosti, 30) Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Dkt. Athumani Kihamia amesema mbali na kumuengua mgombea huyo, Tume imeamua kuwa wagombea saba (7) wataendelea na uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Septemba 16.

Mbali na uamuzi wa rufaa hizo, Dkt. Kihamia amevikumbusha vyama vya siasa na wagombea wanaoshiriki katika uchaguzi huo,  kuzingatia Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015, wakati wote wa kampeni na hata siku ya uchaguzi.

Dkt. Kihamia alifafanua kuwa uamuzi wa rufaa hizo umezingatia matakwa ya kanuni ya 29(3), (4) na (5) ya Kanuni za Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (Uchaguzi wa Madiwani) za mwaka 2015.

“Tume, ilipokea, ilijadili na kufanya maamuzi ya Rufaa hizo nane (8) ambazo kati ya hizo rufaa, mbili (2) zilipinga kuondolewa kugombea na kutaka kurejeshwa kugombea na rufaa sita (6) zilikuwa zikipinga wagombea walioteuliwa”, alisema Dkt. Kihamia na kuongeza kuwa:

“Tume imeamua kuwa wagombea saba (7) wataendelea na uchaguzi na mgombea mmoja ameenguliwa na hivyo kutoendelea kuwa mgombea.Taarifa za maamuzi ya rufaa hizo, zimetumwa kwa wahusika kupitia kwa Wasimamizi wa Uchaguzi wa Halmashauri husika”.

Aliongeza kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilipokea rufaa nane (8) kutoka kwa wagombea udiwani wa Kata za Sisimba, Maanga, Nsalaga na Iwambi katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya.

Alisema wagombea wengine walitoka Kata ya Nkuyu katika Halmashauri ya Wilaya ya Kyela; Kata ya Kizota katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma na Kata ya Mwanhuzi katika Halmashauri ya Wilaya ya Meatu.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi