[caption id="attachment_29028" align="aligncenter" width="750"] Sehemu ya wakazi wa kata Zogoali katika wilaya ya Ilala wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (hayupo pichani).
Na Greyson Mwase, Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu ametoa onyo kwa matapeli wanaojitokeza kwa kujifanya maafisa wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na kuwatoza wananchi fedha kama malipo ya kuunganishiwa huduma ya umeme.
Mgalu aliyasema hayo mwishoni mwa wiki katika mikutano aliyoifanya wakati wa ziara yake katika katika kata za Bomba Mbili, Mbondole, Kiboga, Zogoali, Kigezi Buyuni na Chanika zilizopo katika wilaya ya Ilala nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Lengo la ziara yake lilikuwa ni kutembelea maeneo ambayo hayajafikiwa na miundombinu ya umeme, kuzungumza na wananchi na kuweka mikakati ya namna ya kumaliza changamoto hizo kwa kushirikiana na REA na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO)
[caption id="attachment_29030" align="aligncenter" width="750"] Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (kushoto) akinukuu maswali mbalimbali yaliyokuwa yanauliuzwa na wakazi wa kata ya Bomba Mbili iliyopo Ilala jijini Dar es Salaam (hawapo pichani) Kulia ni Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara.Awali, wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi wa kata husika walilalamika kuwepo kwa tabia ya baadhi ya watu ambao wamekuwa wakijitambulisha kwao kama maafisa kutoka REA na TANESCO na kuwachangisha fedha nyingi ili wawaunganishie huduma ya umeme kinyume na taratibu.
Walisema kuwa baada ya kufanya malipo kwa watu hao walishangaa kuona wametoweka na fedha hizo pasipo kuwapatia huduma ya aina yoyote.
Akifafanua kero hiyo, Mgalu alitoa wito kwa wananchi kutoa taarifa katika vyombo vya usalama pindi watu wasiofahamika wanapojitokeza na kudai michango kwa ajili ya kuwaunganishia huduma ya umeme.
Aliongeza kuwa wakandarasi kabla ya kuanza kazi ya kuweka miundombinu ya umeme katika kata husika, wanatakiwa kujitambulisha kwa viongozi wa mtaa ili waweze kutambulishwa kwa wananchi.
Alisema kuwa katika kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma ya umeme Serikali imetoa punguzo kubwa ambapo kila mwananchi aliyepo ndani ya miradi ya REA atatakiwa kuchangia gharama ya shilingi 27,000 tu.
Vilevile aliwataka wananchi kujiandaa kwa kuunganishiwa na huduma ya umeme kupitia REA kwa kutandaza nyaya za umeme kwenye nyumba zao kupitia wakandarasi wanaotambulika na TANESCO