Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mfumuko wa Bei wa Taifa Umepungua Kufikia Asilimia 3.3
Aug 09, 2018
Na Msemaji Mkuu

 Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Jamii Bw. Ephraim Kwesigabo akitoa taarifa ya hali ya mfumuko wa bei kwa mwezi Julai 2018 leo Jijini Dodoma ambapo mfumuko huo umeshuka kwa asilimia 3.3 kwa mwezi Julai 2018 ikilinganishwa na asilimia 3.4 kwa mwezi June 2018.

Na: Lilian Lundo - MAELEZO, Dodoma.

Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwezi Julai, 2018 umepungua hadi kufikia asilimia 3.3 ikilinganishwa na asilimia 3.4  mwezi Juni, 2018.

Hayo yameelezwa leo na Jijini Dodoma na  Mkurugenzi wa sensa na Takwimu za Jamii, Ofisi ya Taifa ya Takwimu Ephraim Kwesigabo alipokuwa akitoa taarifa  ya mfumuko wa bei kwa mwezi Julai mwaka huu.

Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Jamii Bw. Ephraim Kwesigabo akisisitiza kuhusu kuendelea kushuka kwa mfumuko wa bei hapa nchini leo Jijini Dodoma  ikilinganishwa na nchi jirani hali inayoonyesha kuendelea kuimarika kwa hali ya uchumi.

Kwesigabo amesema, kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Julai, 2018 imepungua ikilinganishwa na kasi ilivyokuwa kwa  mwaka ulioishia mwezi Juni, 2018.

"Kupungua kwa mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Julai, 2018 kumechangiwa hasa na kupungua kwa mfumuko wa bei wa baadhi ya bidhaa za vyakula, ambapo bidhaa za vyakula zilizochangia kupungua kwa mfumuko wa bei kati ya Julai, 2017 na Julai 2018 ni pamoja na unga wa mahindi kwa asilimia 9.5, mtama kwa asilimia 17.8, unga wa mihogo kwa asilimia 14.1, matunda jamii ya machungwa kwa asilimia 22.2, maharagwe kwa asilimia 5.8 na mihogo mibichi kwa asilimia 12.5," amefafanua Kwesigabo.

Ameendelea kusema kuwa ni zaidi ya miaka 15 tangu itokee tarakimu kama hiyo ya mfumuko wa bei ambayo iko vizuri kwa uchumi wa nchi.

Meneja wa Takwimu za mazingira na uchambuzi Bibi Ruth Minja (kushoto) akisisitiza kuhusu umuhimu wa takwimu katika kuchochea maendeleo.

Aidha ametaja hali ya mfumuko wa bei kwa baadhi ya  nchi za Afrika Mashariki kama ifuatavyo; Uganda mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Julai, 2018 umeongezeka hadi asilimia 3.1 kutoka asilimia 2.2 kwa mwaka ulioishia mwezi Julai, 2018. Kwa upande wa Kenya mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Julai, 2018 umeongezeka hadi asilimia 4.35 kutoka asilimia kutoka asilimia 4.28 kwa mwaka ulioishia mwezi Juni, 2018.

Mfumuko wa bei wa Taifa unapima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na kaya binafsi nchini.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Bw. Said Ameir akisisitiza jambo wakati wa hafla ya kutoa taarifa ya hali ya mfumuko wa bei kwa mwezi Julai 2018 Jijini Dodoma.

(Picha zote na Frank Mvungi- MAELEZO)

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi