Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mfumo Mpya wa Ununuzi wa Umma Kudhibiti Rushwa - Maswi
Jul 17, 2023
Mfumo Mpya wa Ununuzi wa Umma Kudhibiti Rushwa - Maswi
Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA), Bw. Eliakim Maswi akieleza utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka hiyo na mwelekeo wa utekelezaji wa Mwaka wa Fedha 2023/24 katika mkutano na Waandishi wa Habari leo Julai 17, 2023 kwenye ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) jijini Dodoma.
Na Immaculate Makilika – MAELEZO

Serikali ilifanya maamuzi ya kujenga mfumo mpya wa ununuzi wa umma  kwa njia ya kielektroniki unaojulikana kwa jina la National e-Procurement System of Tanzania (NeST), ambao unapatikana kwa kupitia anuani ya https://www.nest.go.tz.

Hayo yameelezwa leo Julai 17, 2023 jijini Dodoma na Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA), Bw. Eliakim Maswi wakati akielezea utekelezaji wa majukumu ya mamlaka hiyo na mwelekeo wa utekelezaji wa mwaka wa fedha 2023/24.

“Mfumo mpya wa ununuzi kwa njia ya mtandao una lengo la kuhakikisha ununuzi wa umma nchini unazingatia nguzo nne muhimu ambazo ni kuongeza uwazi kwenye ununuzi wa umma, usimamizi mzuri wa fedha za umma, kudhibiti vitendo vya rushwa na ufuatiliaji wa ukidhi wa sheria na uwajibikaji na udhibiti wa ununzi,” alisema Bw. Maswi.

Aliendelea kusema, “kuanzia tarehe 1 Julai 2023, mfumo wa NeST umeanza kutumika rasmi na hii imeenda sambamba na kuzipatia mafunzo Taasisi za Umma na Wazabuni. Kwa mantiki hiyo, taasisi nunuzi zote ikiwa ni pamoja na Wizara, Idara za Serikali, Taasisi zinazosimiwa na Msajili wa Hazina na Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa   zinapaswa kuanza  kutumia  mfumo  mpya kwa shughuli za ununuzi wa umma kuanzia mwaka wa fedha 2023/24”.

Aidha, inaelezwa kuwa kwa takribani miaka minne, Serikali imekuwa ikitumia mfumo wa awali wa TANePS ambao umegubikwa na changamoto mbalimbali. Baadhi ya changamoto hizo ni kutokuwa rafiki kwa watumiaji, kuwa na hitilafu za kiufundi za mara kwa mara na mfumo kuwa na mianya ya kuwezesha taasisi kutotumia mfumo, hivyo kusababisha malalamiko kutoka kwa wazabuni na Taasisi Nunuzi. Wazabuni kulalamika kwa kukosa uwazi, ushindani wa haki lakini kibaya zaidi bidhaa, kazi na huduma kukosa thamani halisi ya fedha na kuleta malalamiko na hoja nyingi za ukaguzi.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi