Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mfuko Mpya wa Hifadhi ya Jamii PSSSF Kuanza Kazi Agosti Mosi Mwaka Huu
Jul 31, 2018
Na Msemaji Mkuu

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera  Bunge Kazi Vijana Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari wakati wa mkutano wa kutangaza tarehe ya kuanza rasmi kufanya kazi kwa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa  Watumishi wa Umma(PSSSF) leo Jijini Dodoma.Kulia ni Mkurugenzi mkuu wa SSRA Dkt. Irene  Isaka.

Na Beatrice Lyimo-Maelezo, Dodoma

Serikali imetangaza rasmi kuanza kutumika kwa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumsihi wa Umma (PSSSF) kuanzia Agosti 1, mwaka huu.

Akizungumza  na vyombo vya habari leo Jijini Dodoma, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amesema kuwa, Serikali imekamikisha maandalizi yote muhimu ya utekelezaji wa Sheria ya PSSSF na imeridhika kwamba Mfuko huo unaweza kuanza kutekeleza majukumu yake.

"Napenda kutangaza rasmi kwamba, kwa mamlaka niliyonayo chini ya kifungu cha 1(1) cha Sheria ya PSSSF nimeteua tarehe 1 Agosti, 2018 kuwa ndiyo tarehe rasmi ya kuanza kutumika kwa Sheria ya PSSSF", alisisitiza mhe. Mhagama.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Bunge Kazi Vijana Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akitangaza rasmi leo Jijini Dodoma tarehe ya kuanza  kufanya kazi kwa mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa watumishi wa Umma (PSSSF)  ambapo mfuko huo unaanza kazi Agosti Mosi mwaka huu.Kushoto ni Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu  Sera na Uratibu Prof. Faustine Kamuzora.

Waziri Mhagama amefafanua kuwa, kutokana na hatua hiyo wafanyakazi wote watakaoajiriwa katika sekta ya umma watasajiliwa katika Mfuko wa PSSSF na wale watakaoajiriwa katika sekta binafsi watasajiliwa katika Mfuko wa NSSF.

Anaongeza kuwa, Wanachama wote ikiwa ni pamoja na wastaafu na warithi waliopo katika mifuko inayounganishwa watahamishiwa katika mfuko wa PSSSF na haki na stahili zao zitaendelea kutolewa na mfuko huo bila kuathiriwa kwa namna yeyote ile

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera  Bunge  Kazi Vijana Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akisisitiza kuhusu hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kuhakikisha kuwa mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa watumishi wa Umma (PSSSF)  unaanza  kutekeleza majukumu yake bila kuathiri huduma kwa wanachama wa mifuko iliyounganishwa.

Akizungumzia rasilimali, vitega uchumi, madeni, mifuko ya hiari na mikataba iliyokuwa chini ya mifuko inayounganishwa  Waziri Mhagama amesema itahamishiwa katika Mfuko mpya wa PSSSF.

Pia Waziri Mhagama amewatoa hofu ya kupoteza ajira watumishi wote wa mifuko iliyounganishwa  kwa kuwa watahamishiwa katika mfuko mpya ambako uongozi wa mfuko huo utawapangia majukumu yao kwa kuzingatia muundo wa taasisi.

Kuondoa sintofahamu Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi ya Mifuko ya Hifadhi za Jamii (SSRA) imeandaa mkakati maalumu wa kutoa elimu kwa umma kuhusu sheria na kanuni za PSSSF ili kuhakikisha kwamba wanachama na wadau wote wa sekta ya hifadhi ya jamii wanakuwa na uelewa sahihi wa sheria hizo na mabadiliko yaliyofanyika.

Mbali na hayo, Waziri Jenista ameteua wajumbe wa Bodi ya Mfuko huo ambao ni Bi. Leah Ulaya, Bw. Rashidi Mtima, Dkt. Aggrey Mlimuka, Bi. Stella Katende, Bw. Thomas Manjati, Bw. Henry Katabwa, Bi. Suzan Kabogo pamoja na Bw. Jacob Mwinula.

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa watumishi wa Umma  (PSSSF) Bw. Eliud Sanga (katikati) akisisitiza kuhusu hatua watakazochukua kuhakikisha kuwa mfuko huo mpya unatatua changamoto zilizokuwepo awali katika mifuko iliyounganishwa kuunda mfuko huo.

(Picha zote na Frank Mvungi- MAELEZO)

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi