Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amemuagiza Katibu Mkuu wa Sekta ya Ujenzi, Balozi Aisha Amour, kuhakikisha anasimamia uundwaji wa sheria ya majengo na nyaraka za viwango na vipimo vya majengo ya Serikali ili kukamilika haraka kwa lengo la kuongeza nguvu katika utekelezaji wa miradi nchini.
Agizo hilo amelitoa jijini Dodoma wakati akizindua Bodi ya Nane (8) ya Wakurugenzi ya Bodi ya Usajili ya Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB), ambapo amesisitiza kuwa uwepo wa sheria hiyo utapelekea miradi ya majengo kutekelezwa kwa haki na usawa.
“Sisi kama Serikali hatuwafanyii haki wa Tanzania, ni miaka mitano (5), sasa tunalizungumzia jambo hili, hivyo naagiza Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC), ambao wamepewa jukumu la uundwaji wa sheria ya AQRB kukamilisha haraka iwekanzavyo sheria hiyo”, amesisitiza Prof. Mbarawa.
Amefafanua kuwa uwepo wa sheria hizo na miongozo hiyo katika utekelezaji wa miradi mbalimbali nchini utasaidia kumaliza changamoto za kutokuwepo kwa makadirio halisi katika utekelezaji wa miradi kama ya majengo na barabara.
Aidha, amewataka wataalam wazawa wa kada ya Wabunifu Majengo na Makadiriaji Majenzi nchini kuungana pamoja na kushirikiana ili ushiriki wa wataalamu katika miradi mikubwa uwe wa kutosha.
“Hivi sasa tunaona miji na majiji yetu yakiwa na miundombinu inayovutia ikiwemo majengo makubwa yanayopendeza yanayofanywa na Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi Wazawa na kutoa matokea chanya hivyo shirikianeni ili mpate zabuni za kutekeleza miradi mingi zaidi”, amesema Waziri Mbarawa.
Ameitaka Bodi hiyo kufanya kazi kwa uadilifu, weledi na bidii ya hali ya juu kwa maslahi ya Taifa ikiwa ni pamoja na kuweka sera na mikakati itakayoiongoza na kuishauri menejimenti ya AQRB katika kutekeleza majukumu ya Taasisi hiyo kwa kuzingatia sera na miongozo ya Serikali kupitia Wizara hiyo katika kutoa huduma kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Mbunifu Majengo Dkt. Ludigija Bulamile, amesema kuwa Bodi hiyo itaangalia hasa kwa nia ya kujifunza mwelekeo wa tathmini za kitaalam katika kupunguza gharama za utekelezaji wa miradi na ushirikishwaji wa wataalam katika miradi mikubwa kwa lengo la kuongeza kasi ya maendeleo nchini.
Naye, Msajili wa Bodi ya AQRB, Arch. Edwin Nnunduma, amesema kuwa Bodi hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uelewa mdogo wa waendelezaji majenzi kuhusu umuhimu wa kutumia wataalam na Kampuni zilizosajiliwa na Bodi kubuni na kusimamia miradi ya ujenzi.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.