Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Gerson Msigwa, amesema kuwa mazingira ya amani na utulivu yamechangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa shughuli za kiuchumi katika Mkoa wa Morogoro.

Amesema hayo Mei 31, 2026 wakati akizungumza na waandishi wa habari katika
eneo la Bwawa la Kidunda kuhusu mafanikio ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati katika Mkoa huo.

“Idadi ya viwanda vya kati imeongezeka kutoka viwanda 23 mwaka 2021 hadi viwanda 63 mwaka 2026, ikiwa ni ongezeko la viwanda 40. Idadi ya viwanda vidogo na vidogo sana imeongezeka kutoka viwanda 1,049 mwaka 2021 hadi 3,147 mwaka 2026, sawa na ongezeko la viwanda 2,098,” amesema Bw. Msigwa.
Katika sekta ya viwanda vikubwa, Morogoro imeendelea kudumisha uwekezaji wake huku ikiwa na jumla ya viwanda vikubwa 38 tangu mwaka 2021.

Aidha, ukuaji huo umeenda sambamba na kuongezeka kwa biashara rasmi zinazomiliki leseni, ambapo idadi ya biashara hizo imeongezeka kutoka 12,656 mwaka 2020 hadi 28,626 mwaka 2026, sawa na ongezeko la biashara 15,970.
Matokeo ya ukuaji huo pia yameonekana katika ukusanyaji wa mapato ya halmashauri. Kiasi cha shilingi bilioni 8.42 kilikusanywa katika mwaka wa fedha 2025/26 hadi Februari 2026 kutoka kwenye biashara zilizopo katika halmashauri mbalimbali za mkoa huo, ikilinganishwa na shilingi bilioni 1.18 zilizokusanywa mwaka 2021.

Ongezeko hilo la viwanda, biashara na mapato linaendelea kutoa ushahidi wa mazingira bora ya uwekezaji, usalama na utulivu wa kisiasa unaoifanya Morogoro kuwa kitovu muhimu cha viwanda na biashara nchini.
Ukuaji huo unatarajiwa kuongeza ajira, kuchochea uzalishaji wa bidhaa za ndani na kuimarisha mchango wa sekta binafsi katika maendeleo ya uchumi wa Mkoa wa Morogoro na Taifa kwa ujumla.