Na Mbaraka Kambona,
Serikali imesema ipo katika mchakato wa kutengeneza viwango vya kitaifa vya ubora na usalama wa mazao ya Mwani na Dagaa ili kuyapa mazao hayo fursa pana ya masoko ya uhakika ndani na nje ya nchi.
Hayo yalisemwa na Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah alipokuwa akifungua mkutano wa Wadau kuhusu mjadala wa viwango vya mazao ya Dagaa na Mwani uliofanyika jijini Dar es Salaam Agosti 24, 2020.
Dkt. Tamatamah alisema kuwa kutengenezwa na kuanzishwa kwa viwango vya kitaifa vya ubora na usalama wa mazao hayo ya uvuvi kutaimarisha na kukuza soko la kitaifa na kimataifa la bidhaa zinazotokana na mazao hayo ya uvuvi.
“Mazao ya dagaa na mwani kwa muda mrefu yamekuwa hayana viwango vya ubora jambo ambalo limekuwa likifanya bidhaa hizo kutokutambulika katika soko la kimataifa ndio maana sasa serikali imeamua kutengeneza viwango vya ubora vya mazao ya uvuvi hasa kwa mazao hayo ili yaweze kupata masoko yenye uhakika ndani na nje ya nchi,”alisema Dkt. Tamatamah.
Alisema kuwa uvuvi wa dagaa pamoja na ukulima wa mwani ni muhimu kwa uchumi wa jamii inayoishi Pwani na taifa kwa ujumla huku akisema kuwa kilimo cha mwani peke yake kinawahusisha takribani wakulima elfu tatu (3000) wengi wao wakiwa ni wanawake.
“Kwa mwaka 2019/2020 kiasi cha tani 1449 za Mwani zilizalishwa na kati ya hizo, asilimia 10 zilitumika hapa nchini katika kutengeneza bidhaa mbalimbali zikiwemo sabuni na aslimia 90 zilisafirishwa kwenda nje ya nchi zikiwemo nchi za China, Marekani, Canada, Uingereza, Denmark na Ufaransa,”alifafanua Dkt. Tamatamah
“Kwa upande wa Zanzibar, uzalishaji wa Mwani umefikia takriban tani 35000 na ndio bidhaa ya pili inayosafirishwa kwa wingi kwenda nje ya nchi,”aliongeza
Dkt. Tamatamah aliendelea kueleza kuwa kutokana na umuhimu huo ni dhahiri kwamba kuna haja ya kuwepo kwa viwango vya ubora na usalama ili wafanyabiashara waweze kuyafikia masoko mbalimbali duniani.
“ Kupitia mradi wa SWIOFish ulio chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) wameweza kuandaa viwango viwili ambavyo ni TBS/AFDC 23 kwa ajili ya unga wa Dagaa na TBS/ AFDC (5714) kwa ajili ya Mwani mkavu,”alibainisha Dkt. Tamatamah
Naye Mkulima wa Mwani, Wilayani Bagamoyo, Mzee Machao Ally Jingalao alisema katika mkutano huo kuwa hatua hiyo ya Serikali ya kutengeneza viwango vya ubora kwa ajili ya mazao hayo ya uvuvi ni hatua nzuri ya kuelekea uchumi wa viwanda.
“Naiomba serikali iongeze nguvu katika kuimarisha biashara hii ya mazao ya uvuvi kwani ikisimamiwa vizuri itasaidia sana kuiongezea mapato nchi na kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja,”alisema Jingalao
Meneja wa Kampuni ya Uwekezaji katika zao la Mwani, Mariculture, Roger Valle Morre aliiomba Serikali kulinda wawekezaji katika zao la Mwani dhidi ya watu wanaojiingiza katika biashara hiyo bila kuwa na vibali.