Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba amewaagiza baadhi ya mawaziri alioambatana nao wabakie mkoani Tanga ili kufuatilia masuala yaliyoibuliwa na wananchi na kuyatafutia ufumbuzi.
Masuala hayo yametokana na hoja zilizoibuliwa kwenye mikutano ya hadhara na wabunge wa Mkoa wa Tanga na wananchi mbalimbali kwenye sekta za ardhi, mifugo, kilimo, maji, elimu na barabara.

Ametoa agizo hilo Februari 17, 2026 wakati akizungumza na wakazi wa Soni, Bumbuli katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye stendi ya Soni, wilayani Lushoto, mkoani Tanga.
Awali, akijibu hoja kuhusu ubovu wa barabara wilayani Lushoto, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshatoa kibali cha kuanza ujenzi wa pande mbili wa barabara ya Soni - Bumbuli- Dindira hadi Old Korogwe.
“Barabara hii ilishatangazwa na sasa tunakamilisha taratibu za wakandarasi. Zikiwa tayari, mmoja ataanzia Soni kwa kujenga kilometa 22 na mwingine ataanzia Old Korogwe (KwaMeta hadi KwaShemsi) kwa kujenga kilometa 9.5,” amesema.

Amesema barabara ya sasa ya kutoka Mombo - Soni hadi Lushoto yenye urefu wa km. 32 imeshafanyiwa usanifu na inatafutiwa fedha ili iweze kufanyiwa upanuzi.
Naye Naibu Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa David Silinde amesema Msajili wa Hazina anamalizia uhakiki wa madeni ya zamani ya wakulima wa chai waliokuwa wanadai malipo katika kiwanda cha chai cha Mponde na kuongeza kuwa katika kipindi cha hivi karibuni hakuna madeni yoyote yaliyolimbikizwa.

Amesema kiwanda hicho ambacho kinahudumia Halmashauri mbili za Bumbuli na Korogwe, kinafanyiwa mpango wa kupata line nyingine ya uzalishaji ili kupunguza mlundikano wa majani ya chai yaliyovunwa. Amesema Bodi ya Chai imeshanunua kiwanda kingine huko Korogwe ambacho kinatarajiwa kuanza kazi kabla ya Juni, mwaka huu ili kisaidie kupunguza mzigo unaoenda kiwanda cha Mponde.