Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mavunde Ataka Mpango wa Matumizi ya Ardhi Kujumuisha Mashamba Makubwa Badala ya Makazi Pekee
Oct 19, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Munir Shemweta, WANMM Shinyanga

Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Anthony Mavunde ametoa rai kwa Watendaji wa Serikali kuhakikisha yale maeneo yote ambayo migogoro ya ardhi imetatuliwa yanapangiwa mipango ya matumizi ya ardhi kwa kujumuisha maeneo ya mashamba makubwa ya kilimo badala ya kupanga maeneo ya makazi tu peke yake.

Naibu Waziri Mavunde ametoa kauli hiyo jana wàkati akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Lyamidati mkoani Shinyanga wakati Kamati ya Mawaziri nane wa Wizara za Kisekta wanaoshughulikia migogoro ya matumizi ya ardhi ya vijiji 975 walipofika eneo hilo.

"Nitoe rai yale maeneo ambayo migogoro yake ya matumizi ya ardhi imetatuliwa basi iwekewe matumizi bora ya ardhi  ili mashamba makubwa yasisahaulike na wakulima wapate maeneo ya kutosha walime, mwisho wa siku waisaidie nchi kukuza uchumi wao mtu mmoja mmoja, uchumi wa kaya na taifa kwa ujumla’’. Alisema Mavunde

Badala ya maeneo ambayo utatuzi wake umefanyika kutengwa kwa ajili ya makazi peke yake ni lazima wataalamu wasimamie mipango ya matumizi bora ya ardhi kwa kuhakikisha wanaingiza maeneo makubwa ya mashamba ya kilimo kwa sababu Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amekuja na mpango wa kuwa na mashamba makubwa ya pamoja (block farms) ili kusaidia kukuza sekta ya kilimo kufikia malengo yake ya kukua kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030.

Kwa mujibu wa Mavunde, mashamba hayo makubwa ya pamoja yatasaidia kurahisisha utoaji wa huduma za ugani kwa wakulima hasa katika mbinu bora za kilimo cha tija na usambazaji wa teknolojia mbalimbali za kilimo ili kusaidia kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo.

‘’Serikali ina mpango wa kuwa na mashamba makubwa ya pamoja 10,000 kufikia mwaka 2030 na kwa sasa sasa hivi nchi nzima ina jumla ya mashamba makubwa ya pamoja zaidi ya 110," alisema Mavunde

Kamati ya Mawaziri nane wa Wizara za kisekta iko katika ziara ya kutembelea mikoa mbalimbali kwa lengo la kutoa mrejesho wa Maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhususiana na utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975, tayari katika awamu hii ya pili kamati hiyo imeshatembelea mikoa ya Rukwa, Katavi, Kigoma, Simiyu na Shinyanga.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi