Juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuhamasisha matumizi ya TEHAMA kwenye shughuli mbalimbali nchini, zimewezesha Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kupunguza muda wa kuchakata madai ya watoa huduma za afya kutoka siku 120 hadi siku 45.
Hayo yamebainishwa leo Machi 10, 2025 jijini Dodoma wakati Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Dkt. Irene Isaka akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu utekelezaji wa Mfuko huo ndani ya miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita ikiwa ni programu inayoratibiwa na Idara ya Habari - MAELEZO.
Dkt. Irene ameeleza kuwa, hapo awali uchakati wa madai ulianzia kwa kujaza fomu ndipo mchakato wa NHIF uanze, kwa sasa NHIF inatumia mfumo uitwao "Online Claim System" ambao unatumika kufikisha ombi la madai ndani ya masaa 24. Pia, mfumo huo una uwezo wa kuchakata madai kwa haraka na kuondoa viashiria vyote vya udanganyifu.
"Kabla ya Serikali ya Awamu ya Sita kuingia madarakani, mwaka 2020 mpaka 2021 mwanzoni, NHIF ilikuwa inatumia siku 120 kuchakata dai hadi kuilipa hospitali au kituo cha afya kilichotoa huduma lakini kwa sasa NHIF inatumia siku 45, pia Daktari mmoja wa NHIF alikuwa akichakata folio 800 kwa siku lakini kwa sasa anaweza kuchakata folio 1000 kwa dakika 45, ndiyo maana kwa sasa madai ya watoa huduma yanalipwa kwa wakati", amesema Dkt. Irene.
Dkt. Irene amefafanua kuwa, matumizi ya mifumo ya TEHAMA yameleta matokeo mazuri ambapo yameiwezesha NHIF kusajili wanachama milioni 2.2 huku katika kipindi cha miezi 6 kuanzia Julai hadi Disemba, 2024 NHIF ilisajili wanachama 284,543.
Vilevile, NHIF imeongeza ukusanyaji wa michango hadi kufikia shilingi trilioni 2.3 ambapo asilimia 92 ni michango ya wananchama, asilimia 7 ni pato la uwekezaji na asilimia 1 ni mapato kutoka vyanzo vingine.
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya unawafikia asilimia 8 ya Watanzania huku vituo vya afya vilivyosaijiliwa ambavyo vinalipwa na NHIF ni 10,004 nchi nzima.