Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Matinyi Atangaza Siku Rasmi Kuaga Mwili wa Lowassa
Feb 14, 2024
Matinyi Atangaza Siku Rasmi Kuaga Mwili wa Lowassa
Mkurugenzi wa Idara ya Habari - Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Ndg. Mobhare Matinyi akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam kuhusu siku rasmi ya kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (2005-2008), Mhe. Edward Lowassa
Na Ahmed Sagaff – Maelezo

Msemaji Mkuu wa Serikali, Ndg. Mobhare Matinyi ametangaza siku rasmi ya kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (2005-2008), Mhe. Edward Lowassa anayetarajiwa kuzikwa huko Monduli mkoani Arusha, Jumamosi ya Februari 17, 2024.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Ndg. Matinyi amesema Jeshi la Ulinzi wa Wananchi Tanzania (TPDF) litapiga mizinga 17 wakati mwili wa Hayati Lowassa utakapokuwa ukiteremshwa kaburini.

“Kamati ya kitaifa ya mazishi chini ya mwenyekiti wake Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa inaendelea kukumbushia kuwa siku ya Ijumaa ndio itakayokuwa siku rasmi kwa waombolezaji wote kutoa heshima zao za mwisho na kuiacha siku ya jumamosi kwa ajili ya familia, viongozi wa kitaifa wakiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kufanya hivyo,” amearifu Ndg. Matinyi.

Pamoja na hilo, Ndg. Matinyi amefahamisha kuwa viongozi wa kimila wa jamii ya kimasai watapata fursa ya kuaga mwili wa Hayati Lowassa na kutoa salamu za rambirambi siku ya Ijumaa.

“Ibada takatifu ya mazishi itafanyika Jumamosi na itaongozwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT),” ameeleza Ndg. Matinyi.

Sambamba na hayo, Ndg. Matinyi amesema mwili wa Hayati Lowassa utasafirishwa kutoka Dar es Salaam kwenda Arusha siku ya Alhamisi kutokea Hospitali ya Jeshi Lugalo kupitia Uwanja wa Ndege wa Kitaifa wa Julius Nyerere (JNIA) hadi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Kilimanjaro (KIA).

“Baadae kesho msafara utapita katika barabara za jijini Arusha kuelekea kijijini kwa Hayati Lowassa Ngarash, Monduli mkoani Arusha,” ameeleza.

Lowassa amefariki Februari 10, 2024 katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) alipokuwa akipatiwa matibabu chini ya usimamizi maalum unaotokana na maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan ambaye mara kwa mara alikuwa akihitaji kujua hali ya afya ya Hayati Lowassa.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi