Mkurugenzi wa Idara ya Habari - Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Ndg. Mobhare Matinyi amesifu idadi ya wawekezaji wa kigeni waliopo mkoani Mtwara.
Akizungumza leo mjini Mtwara, Ndg. Matinyi amesema idadi hiyo inaweza kusukuma mbele maendeleo ya mkoa huo huku akiwataka vijana kuchangamkia fursa za ajira.
“Kwa kadiri Mhe. Mkuu wa Mkoa ulivyouelezea mkoa huu wa Mtwara kuwa ni mkubwa na una vitu vingi vya kimaendeleo mkoa huu unafanya kazi na wawekezaji mbalimbali wa kigeni kama vile wa gesi, kiwanda cha saruji, Bandari ya Mtwara ina mambo makubwa, na nimefurahi kusikia taarifa za kituo cha afya cha Mtange,” amesema Ndg. Matinyi.
Pamoja na hilo, Ndg. Matinyi ameeleza kuwa Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imekuwa ikitoa fedha nyingi mkoani humo kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
"Hakika mnafanya kazi nzuri kuhakikisha fedha zilizotolewa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya maendeleo Mtwara, hazipotei bali zimefanya kazi iliyotukuka,” amehitimisha Ndg. Matinyi.