Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Bw. Mavere Tukai amesema kutokana na maboresho yanayoendelea na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali, mapato ya MSD yameongezeka kutoka shilingi bilioni 315.1 kwa mwaka wa fedha 2021/22, hadi kufikia shilingi bilioni 553.1 kwa mwaka wa fedha 2023/24.
Bw. Tukai amesema hayo leo Machi 19, 2025 katika Ofisi za Idara ya Habari-MAELEZO wakati wa mkutano na Waandishi wa Habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa MSD katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita.
“Mapato ya Bohari ya Dawa yameongezeka kutoka shilingi bilioni 315.1 kwa mwaka wa fedha 2021/22, hadi kufikia shilingi bilioni 553.1 kwa mwaka wa fedha 2023/24, ikiwa ni ongezeko la shilingi bilioni 238 ambayo ni sawa na asilimia 76,” amesema Bw. Tukai
Ameendelea kusema kuwa, katika kipindi cha Julai 2024 hadi Februari 2025, Bohari ya Dawa imepata mapato ya thamani ya shilingi bilioni 400.2 sawa na asilimia 115 ya lengo la kusambaza bidhaa za afya zenye thamani ya shilingi bilioni 346.6.
Aidha, Serikali imeendelea kuimarisha mfumo wa makusanyo ya fedha kutoka vituo vya kutolea huduma za afya kwa kuwezesha MSD kuhudumia vituo hivyo.
“Kutokana na kuimarika kwa utendaji wa Bohari ya Dawa, makusanyo ya fedha kutoka kwenye vituo vya kutolea huduma za afya yameendelea kuongezeka katika kipindi cha Serikali cha Awamu ya Sita ambapo makusanyo yameongezeka kutoka shilingi bilioni 54.2 mwaka 2021/2022 hadi kufikia shilingi bilioni 118.9 mwaka 2023/2024,” amefafanua Bw. Tukai.
Ongezeka la makusanyo ya fedha limetokana na maboresho yanayoendelea yaliyowezesha kupatikana kwa bidhaa nyingi Bohari ya Dawa zinazoendana na mahitaji ya vituo, kuongezeka kwa uwezo wa wateja kulipia bidhaa pamoja na kuimarika kwa mahusiano kati ya MSD na wateja.