Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mapambano dhidi ya Rushwa ni Vita ya Wote
Aug 21, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na: Bushiri Matenda

Seikali imetoa wito kwa wadau mbali mbali kuendelea kuunga mkono mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa nchini ili kuendana na kasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ya kupiga vita rushwa na ufisadi.

Wito huo umeolewa na Mwakilishi wa Kituo cha Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni Bw. Sixmund Begashe  ambae pia ni Msemaji wa Kituo  hicho wakati akiongea na  Waandishi wa Habari leo Jijini Dar es Salaam kuhusu matumizi ya Sanaa na Wasanii katika mapambano dhidi ya rushwa nchini.

“Watanzania na Wasanii wote nchini katika maeneo yao hawana budi ya kufanya jitihada za dhati ili kupambana na kutokomeza kabisa vitendo ya rushwa. Rushwa ni changamoto kubwa inayosumbua na hata kurudisha nyuma maendeleo ya Watanzania na Tanzania kwa ujumla” alisema Bw. Begashe.

Alieleza kuwa Kituo hicho ambacho ni moja ya vituo vya Makumbusho ya Taifa nchini kwa kushirikiana na Ubalozi  wa Uswisi Nchini kupitia programu maalum ya sanaa ijilikanayo kama MUSEUM ART EXPLOSION  ya kila mwisho wa juma la mwezi, wameamua kutumia sanaa  na wasanii katika kuelimisha jamii juu ya changamoto ya rushwa nchini na namna bora ya utatuzi wa changamoto hiyo.

“Malengo ya kuwa na program hii ni kuhamasisha wasanii ili kutumia kazi zao za sanaa za ufundi na majukwaa ili kuelimisha jamii juu ya madhara ya rushwa na njia ya kupambana na vitendo hivyo na pia kufikisha ujumbe utakaoishi kwa muda mrefu kuhusu rushwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine”, alisisitiza Bw. Begashe.

Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Sanaa na Ufundi Tanzania Bw. Adrian Nyangamalle alisema Sanaa ni chombo muhimu katika kupitishia habari mbali mbali katika jamii hivyo sanaa ikitumika vizuri itaweza kutokomeza vitendo vya rushwa nchini.

“Wasanii kama kama ilivyo jamii nyingine nao wamekumbwa na mdudu rushwa. Rushwa haijawahi kumwacha mtu salama kwani inaathili hadi watu ambao sio wasanii” alisema Bw. Nyangamalle.

Aliongeza kuwa katika kudhihirisha umuhimu wa kazi ya sanaa kwa Taifa, Kinyago cha Ujamaa ambacho  ni moja ya falsafa ya Ujamaa na Kujitegemea, kimekuwa kikitumika kama zawadi inayotolewa na Serikali kwa viongozi wa Kimataifa wanaotembelea nchini wenye lengo la kuwaonesha umoja wetu.

Kituo cha Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni kinatarajia kufanya maonesho Jijini Dar es Salaam na mikoa mingine nchini kwa kutumia kazi za Sanaa za michezo ya kuigiza, vinyago, picha na mavazi wenye lengo la kuelimisha jamii juu ya vitendo vya rushwa na kubaini njia sahihi za kukabiliana na vitendo hivyo.

Wananchi  wametakiwa kujitokeza kwa wingi ili kujifunza na kukutana na Maafisa wa  Tasisi ya Kuzuia Kupambana na Rushwa Nchini (TAKUKURU) ambapo watapokea kero na malalamiko mbalimbali yahusiyo masuala ya rushwa katika maeneo yote ambayo maonesho hayo yatafanyika.

Hivyo maoenesho hayo katika Mkoa wa Dar es Salaam yanatarajiwa kuanza mwishoni mwa wiki hii katika manispaa zake za Ilala, Temeke na Ubungo na baadae maonesho hayo yataendelea katika mikoa ya Pwani, Morogoro,Iringa, Njombe, Songea, Tanga, Kilimanjaro na baadae mkoani Arusha.

Miongoni mwa majukumu ya Kituo cha  Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni ni kufanya kazi za kutafiti, kuhifadhi, kuelimisha na kuvionesha vitu vyenye thamani kubwa katika urithi wa utamaduni wa Mtanzania, Pia inajishughulisha na uandaaji wa program mbalimbali zenye lengo la kuanisha changamoto katika jamii ili iweze kujifunza njia mbalimbali za kukabiliana nazo mfano suala la tatizo la rushwa nchini.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi