Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Manispaa ya Tabora Yaagizwa Kuwaondoa Wavamizi wa Viwanja vya CCM na Watu Wengine.
Oct 10, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na: Tiganya Vincent

SERIKALI imeuagiza  Uongozi wa Manispaa ya Tabora kuhakikisha wanamaliza tatizo la uvamizi wa Viwanja vinavyomilikiwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) na vile vinavyomilikiwa na Taasisi nyingine na watu binafsi ili waweze kuviendeleza.

Kauli hiyo imetolewa jana mjini Tabora na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mabula wakati alipotembelea Ofisi za Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Tabora akiwa katika ziara ya siku moja katika Chuo cha Ardhi Tabora.

Alisema kuwa ni vema Halmashauri zote zikahakikisha zinaondoa migogoro ya ardhi kwa kuhakikisha watu wenye maeneo yao ambayo yamevamiwa au kugawia watu wengine ambao sio wamiliki kihalali wanawaondoa na kuwarejeshea watu au Taasisi ambazo ndio zinazomiliki maeneo husika.

Naibu Waziri huyo alisema kuwa Mamlaka zinapochelewa kutatua migogoro ya ardhi zinasababisha tatizo kuzidi kuwa kubwa na kusababisha usumbufu kwa wamiliki halali.

Aidha Naibu Waziri huyo alizishauri Taasisi na watu binafsi wanaomiliki maeneo yao kihalali kuhakikisha wanaweka alama ikiwa ni pamoja na kupanda mimea hata kama maeneo yao bado hajapimwa ili kupunguza migogoro.

Awali akitoa salamu za Chama cha Mapinduzi(CCM) Mkoa wa Tabora kwa kiongozi huyo, Katibu wa CCM Mkoa wa Tabora Janeth Kayanda aliomba Serikali kuwasaidia kuwarudishia viwanja vyao sita ambavyo vilivyomilikishwa kwa watu wengine.

Alisema kuwa kitendo hicho kimesababisha Chama kishindwe kupanga mipango mbalimbali ya kuendeleza maeneo husika kwa sababu ya kuwepo na wavamizi hao na hivyo kumuomba kusaidia katika kutafutia ufumbusi wa viwanja vyao ili waweze kutekeleza mipango waliokusudia katika viwanja hivyo.

Katika hatua nyingine Katibu huyo wa Mkoa alimwomba Naibu Waziri kuangalia jinsi ya kuwasaidia baadhi ya wakazi wa Tabora ambao ni miongoni mwa wale 402 ambao nyumba zao zinatarajia kubomolewa kupitisha ujenzi wa reli ya kisasa.

Alisema kuwa baadhi yao walipewa kimakosa  viwanja hivyo na Mamlaka zinazohusika na ugawaji wa viwanja na kufuata taratibu zote na kulipia lakini hivi sasa wanatakiwa waondoke lakini miongoni hawana tena uwezo wa kujenga hata kama wakipewa viwanja.

Naye Mkuu wa Mkoa Tabora Aggrey Mwanri alimwakikishia Naibu Waziri huyo kuwa atahakikisha kuwa wavamizi wote wa viwanja wa chama na vile vya taasisi nyingine na watu binafsi wanaondolewa na kupewa wamiliki wake kihalali.

Kufuatia hali hiyo alimwagiza Mkurugenzi Mteandaji wa Manispaa ya Tabora kuhakikisha ndani ya wiki mbili watu wote waliovamia viwanja vya Chama wanaondoka nay eye anapata taarifa.

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi yuko mkoani Tabora kwa ziara ya kikazi katika Chuo cha Ardhi ya siku moja ambapo baada ya hapo atakwenda Singida na Morogoro.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi