Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Manispaa ya Tabora Tengeni Eneo la Maharusi Kupanda Miti-Mwanri.
Jun 06, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na Tiganya Vincent- RS Tabora.

Uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora umeagizwa kutenga maeneo (bustani) maalum kwa ajili Maharusi kutoka madhehebu mbalimbali  kushiriki zoezi la  kupanda miti ili kuweka ukumbusho wa siku ya ndoa yao.

Agizo hilo limetolewa jana  na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri wakati wa maadhimisho ya siku ya mazingira duniani ambapo kimkoa yalifanyika katika Manispaa ya Tabora.

Alisema kuwa hatua hiyo itasaidia Maharusi kutoka madhehebu mbalimbali kuweka kumbumbuku ya kihistoria ambayo itakuwa faida kwao na kizazi chao.

Mwanri alisema kuwa Harusi hizo zitapendeza zaidi kama wanandoa mkoani humo wataamua kuunga mkono zoezi linaloendelea la upandaji miti kwa kupiga picha wakipanda miti na kuhakikisha zoezi hilo linakuwa endelevu mkoani humo.

Mkuu huyo wa Mkoa alisema kuwa maharusi hao baada ya kupanda miti na kuitunza wanaweza kuweka kumbukumbu ya majina yao ili kuonyesha mchango wao katika utunzaji wa mazingira siku walipoamua kuanza maisha mapya.

Aliongeza kuwa eneo hilo linaweza likapangiliwa vizuri na kulifanya kuwa kivutio sio tu kwa wenyeji hata wageni na hivyo kuingizia Manispaa mapato kupitia tozo za utalii.

“Kumbukumbu nzuri kwa Bwana na Bibi harusi ambayo wanayoweza kuipatia jamii inayowazunguka na kubaki katika historia ya maisha yao ni kuhakikisha kuwa siku ile ya ndoa wanapanda miti na kuitunza ili ije iwe hamasa kwa watoto wao watakaojaliwa na Mwenyezi Mungu,” alifafanua Mwanri.

Kauli mbiu ya maadhimisho ya siku ya mazingira Kitaifa kwa mwaka huu ni “Hifadhi za Mazingira Muhimili wa Tanzania ya Viwanda”.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi