Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea, Dkt. Frederick Sagamiko amewaeleza Waandishi wa Habari kuwa kilimo sasa katika Manispaa ya Songea ni cha kimkakati kwa ajili ya biashara na chakula.
Dkt. Sagamiko ameyasema hayo leo kwenye mkutano wa Mkuu wa Mkoa na Waandishi wa Habari uliohusu ripoti ya utekelezaji wa miradi ya serikali katika mkoa wa Ruvuma.
Akifafanua, Dkt. Sagamiko amesema uzalishaji wa mazao umeongezeka kutoka tani 66,870 kabla ya uongozi wa Awamu ya Sita hadi tani 91,394.8 katika Awamu hii ya Sita, hii inamaanisha uhakika wa chakula nchini na ziada inatumika kibiashara.
Dkt. Sagamiko akielezea kuhusu elimu msingi na sekondari amesema kwa Manispaa ya Songea anaishukuru serikali kwa kuwawezesha kupiga hatua kubwa waliyofikia.
“Kabla ya uongozi wa Awamu ya Sita zilikuwepo shule za msingi 86 na hivi sasa ziko shule 101 zimesaidia kuboresha ufaulu na kuondoa adha ya wanafunzi kubanana madarasani,” amefafanua Dkt.
Sagamiko.
Alikazia akisema, "Tulikuwa na shule 41 kabla na sasa hivi ziko shule 43 ongezeko hilo limesaidia kupunguza msongamano na kuongeza ufaulu ambao umepanda kutoka asilimia 56.9 hadi asilimia 92 kwa kidato cha nne na asilimia 100 kwa kidato cha sita.”
Fauka ya hayo, Dkt. Sagamiko alitaja sekta zingine ni afya kuwa imeboreshwa ikilinganishwa na hapo awali, tuna hospitali tatu kubwa ambazo zimepunguza vifo hasa kwa mama na mtoto, vituo vya afya kutoka sita hadi tisa, zahanati 34 hadi 37 hali inayofanya kuimarika kwenye sekta ya Afya.