Na: Tiganya Vincent
Uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora umewataka walengwa wa mkopo wa asilimia 10 unaotokana na mapato ya ndani kujitokeza kuomba kwani fedha za kuwakopesha zipo.
Kauli hiyo imetolewa jana na Naibu Meya wa Manisapaa hiyo Yahaya Muhamali wakati wa mkutano wa hadhara wa kuwatangazia wananchi, wafanyabiashara na Wajasiriamali wa Mkoa juu ya Jukwaa la Biashara na Uwekezaji litakalofanyika mwishoni mwa Mwezi Novemba mwaka huu.
Alisema kuwa Manispaa hiyo inazo milioni 30 ambazo zipo kwa ajili ya malengo ya kuvikopesha vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu lakini hadi hivi sasa vikundi vina suasua kuomba fedha hizo.
Muhamali alitoa wito kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ambao bado hawajajiunga pamoja kufanya hivyo na kusajili vikundi vya kwa ajili kwenda Manispaa ya Tabora ili wapatiwe taratibu za kupatiwa mkopo ambao utawasaidia kuendesha shughuli zao na kuondokana na umaskini.
Naibu Meya huyo alisema baadhi yao wamekuwa wakiogopa kwenda kukopa fedha hizo kwa sababu mbaya za historia ya baadhi ya Taasisi ambazo zinaendesha biashara ya kukopesha wananchi kwa kuwadai riba kubwa na wakati mwingine kufisiliwa.
Alisema mikopo wanayotoa ni tofauti na ile ya Taaisisi za watu binafsi zinazokopesha kwani haina masharti magumu na wala haina riba.
Muhamali alisema ili kuisaidia jamii kuondoa mtazamo huo , Manispaa ya Tabora imeanza kutoa elimu juu ya matumizi ya fedha za mkopo ili walengwa wengi wachangamkie fedha hizo na watumie fursa hizo kwa malengo waliombea.
Kuhusu wale ambao tayari wameshakopa alitoa wito wa kuhakikisha wanarejesha fedha hizo ili ziweze kunufaisha vikundi vingi na kusisitiza kuwa fedha hizo ni mkopo na sio ruzuku kama wengine wanavyodhani.