Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Makamu wa Rais Ataka Viwanda Kupunguza Uzalishaji Taka
Jun 04, 2017
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_2660" align="aligncenter" width="750"] Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, akipanda mti wa asili kwenye msitu wa Mwalimu Nyerere Kijijini Butiama mkoani Mara wakati wa maadhimisho ya siku ya mazingira duniani ambayo kitaifa imefanyika wilayani Butiama. (Picha na Ofisi ya Mkuu wa mkoa Mara)[/caption]

Na: Jamal Zuberi -RS MARA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Tanzania inaweza kuwa nchi ya viwanda endelevu endapo tu viwanda hivyo vitatumia rasilimali chache kuzalisha bidhaa huku vikipunguza kwa kiwango kikubwa uzalishaji wa taka na kudhibiti uchafuzi wa mazingira.

Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema hayo leo wakati wa kilele cha Madhimisho  ya Siku ya Mazingira Duniani ambayo kitaifa yamefanyika katika wilaya ya Butiama mkoani Mara.

‘Tunaamini kuwa viwanda ni moja ya nyenzo za kutupeleka katika uchumi wa kati kwa haraka na kupunguza umasikini. Malengo hayo hayatafikiwa  iwapo hatutazingatia  sheria na kanuni za utunzaji wa mazingira endelevu,” alisisitiza  Makamu wa Rais.

Alisema kuwa zipo faida nyingi za kuhifadhi na kusisimia mazingira zitakazotokana na Tanzania kuwa na viwanda vingi ambayo pamoja na upatikanaji wa ajira, kuwepo kwa viwanda pia kutaipeleka nchi kwenye uchumi wa kati ambao utawaongezea wananchi wengi kipato na kuondoka na umasikini.

Aidha ametoa wito kwa Watendaji wote nchini kuhakikisha wanasimamia kikamilifu masuala ya hifadhi na mazingira kwa kuokoa mifumo ya ikolojia ili kuwe na maji ya kutosha na kuhifadhi bioanuai, kupanda aina ya miti inayofaa katika maeneo husika na kutokata miti kiholela. Pia amesisitiza uhifadhi misitu na uoto wa asili, kuepuka uchomaji wa moto, kudhibiti uchafuzi wa mazingira utokanao na shughuli za viwanda na uchimbaji wa madini na kilimo kisichokuwa  endelevu.

Makamu wa Rais amewaagiza Watendaji wa kila Mkoa nchini kuhakikisha kuwa wanapanda miche milioni moja na nusu kila mwaka kama walivyoagizwa awali na kuhakikisha kuwa miche hiyo inatunzwa na kukua vema.

Ameeleza kuwa kutozingatia uhifadhi na utunzaji wa  mazingira kunaweza kushababisha kuvurugika kwa mfumo wa kutengemeana kati ya binadamu, viumbe na mazingira na kufanya maisha na vizazi vijao kuwa mashakani.

Kauli mbiu ya  maadhimisho ya siku ya mazingira kitaifa kwa mwaka huu inasema “Hifadhi ya mazingira” ni mhimili kwa Tanzania ya Viwanda”

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi