Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amesema kuwa Wizara hiyo imejipanga kutekeleza Miradi nane ya Maendeleo kwa Mwaka wa Fedha 2022/23.
Ameyasema hayo leo Bungeni jijini Dodoma wakati akisoma hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Ameitaja miradi hiyo kuwa ni; mradi Usimamizi wa Maliasili na Kuendeleza Utalii Kanda ya Kusini, Mradi wa Maboresho ya Usimamizi wa Fedha za Umma, Mradi wa Kukabiliana na Ujangili na Biashara Haramu ya Wanyamapori, Mradi wa Kujenga Uwezo wa Maeneo ya Hifadhi, Mapori ya Akiba na Kikosi Dhidi Ujangili, Mradi wa Panda Miti Kibiashara, Mradi wa Kujenga Uwezo wa Taasisi na Mafunzo ya Misitu na Ufugaji Nyuki, Mradi wa Kuwezesha Mnyororo wa Thamani wa Mazao ya Nyuki, Mradi wa Uendelezaji wa Utalii wa Mikutano na Matukio na Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa dhidi ya UVIKO-19.
“Ninaomba Bunge lako Tukufu liidhinishe jumla ya Shilingi bilioni 624.1 kwa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ambapo kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 443.7 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Shilingi bilioni 180.4 ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo”, amesema balozi Dkt. Pindi Chana.
Kwa upande wa Sekta ya Utalii, Mhe. Balozi Pindi Chana amesema kuwa Wizara itakamilisha Mkakati wa Utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Utalii ya Mwaka 1999 na kuandaa Programu ya Maendeleo ya Utalii nchini.
Aidha, Wizara itabainisha maeneo ya fukwe katika maziwa makuu ya Viktoria, Tanganyika na Nyasa kwa ajili ya uwekezaji na uendelezaji wa shughuli za utalii.
Katika hatua nyingine, Wizara itaendelea kupanga huduma za malazi katika daraja za ubora katika Mikoa ya Kilimanjaro, Mbeya na Mwanza. Sambamba na hilo, Wizara itabaini vivutio vya utalii na fursa za uwekezaji wa shughuli za utalii nchini katika Mikoa ya Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe, Morogoro na Tanga.
Pia, Wizara itaandaa mkakati wa uendelezaji wa utalii wa mikutano na matukio na kuratibu Mkutano wa 65 wa Shirika la Utalii Duniani - Kamisheni ya Kanda ya Afrika (UNWTO 65th CAF Meeting).
Sambamba na hilo, Wizara itaratibu na kushiriki katika matukio yanayohusisha utangazaji utalii ndani ya nchi pamoja na kuendeleza juhudi zilizoanzishwa kupitia programu ya Tanzania – The Royal Tour.
Waziri Pindi Chana ametoa rai kwa Watanzania wote na wadau wa sekta ya maliasili na utalii nchini, kuendelea kushirikiana na Wizara kuhifadhi maliasili, malikale na kuendeleza utalii kwa maendeleo ya Taifa letu na dunia kwa ujumla.