Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Makonda Atoa Rai kwa Walimbwende Kukinadi Kiswahili Duniani
Apr 13, 2026
Makonda Atoa Rai kwa Walimbwende Kukinadi Kiswahili Duniani
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Paul Christian Makonda akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya mashindano ya Miss World yanayoandaliwa na kampuni ya 361 Africa, katika ukumbi wa Bedt Western Hotel, jijini Dodoma.
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul  Makonda, ametoa rai kwa walimbwende wanaoshiriki shindano la Miss World Tanzania kuendelea kuinadi lugha ya Kiswahili duniani ili kuitangaza Tanzania na kuongeza fursa zitokanazo na matumizi ya lugha hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 13, 2026 jijini Dodoma, Waziri Makonda amesema washiriki wa shindano hilo wanapaswa kuitumia nafasi hiyo kama jukwaa la kutangaza utamaduni wa Mtanzania, hususan lugha ya Kiswahili ambayo ni fahari ya Taifa.

Amesema walimbwende hao, ambao ni miongoni mwa washiriki 20 waliowasili jijini Dodoma kwa ziara maalum, wametembelea Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mji wa Serikali Mtumba pamoja na Hospitali ya Benjamin Mkapa.

Aidha, Waziri Makonda ameeleza kuwa mshindi wa taji hilo atakuwa balozi wa Tanzania kimataifa, hivyo anapaswa kuzingatia maadili, utu na utamaduni wa Kitanzania katika kupeperusha bendera ya Taifa.

“Pamoja na mambo mengine, kwenye mashindano haya msisahau kutangaza utamaduni wetu, hasa lugha ya Kiswahili kwani ndiyo fahari kubwa ya Taifa lenu,” amesema Mhe. Makonda.

Ameongeza kuwa mashindano hayo siyo ya kuonesha urembo pekee bali ni “urembo wenye kusudi”, na amewahimiza washiriki kutokata tamaa katika kufikia ndoto na malengo yao.

Katika hatua nyingine, Waziri Makonda amewahimiza Watanzania kushirikiana na wizara yake kwa kuwasilisha mawazo ya ubunifu yatakayosaidia kukuza vipaji na maendeleo ya sekta ya sanaa na utamaduni.

“Wizara imebeba tabasamu na matumaini kwa watu wote. Nawasihi wadau waendelee kuleta mawazo yao ili tushirikiane kurahisisha kazi zao,” amesisitiza.

Fainali ya mashindano ya Miss World Tanzania inatarajiwa kufanyika Aprili 19, 2026 katika Ukumbi wa SuperDome, Masaki jijini Dar es Salaam, ambapo mshindi ataiwakilisha Tanzania katika mashindano ya Miss World yatakayofanyika Septemba mwaka huu nchini Vietnam.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi