Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Makonda Aitaka Taifa Stars Kupambania Heshima ya Taifa AFCON
Dec 24, 2025
Makonda Aitaka Taifa Stars Kupambania Heshima ya Taifa AFCON
Na Baraka Messa – MAELEZO

Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Makonda, ameitaka timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) kuhakikisha inafanya vizuri katika michezo miwili iliyosalia ya AFCON ili kulinda heshima ya taifa licha ya kupoteza mchezo wa kwanza dhidi ya Nigeria.

Akizungumza na wachezaji baada ya mchezo kati ya Taifa Stars na  Nigeria (Super Eagles ) uliochezwa nchini Morocco na kumalizika kwa Stars kufungwa mabao 2-1, Makonda alisema kuwa licha ya matokeo hayo, wachezaji wameonyesha kiwango kizuri cha uchezaji na moyo wa kizalendo.

"Nimepata nafasi ya kuongea na Rais wa CAF, amekiri kuwa kiwango cha mpira Tanzania kinakua, pia nimekaa na Rais wa shirikisho la Nigeria amesema walichokiona uwanjani hawakutarajia kama wangekutana na ushindani mkubwa kama waliokutana nao kutoka kwa Stars " amesema Naibu Waziri

Aidha Mhe. Makonda amesema Taifa Stars wamedhihirisha kuwa Tanzania kuna timu imara huku akiwasihi wachezaji  kuhakikisha wanatumia michezo iliyobaki kupata ushindi na kuendelea kupambania heshima ya bendera ya taifa.

Vile vile, amewataka wachezaji wa timu ya taifa kupeleka hasira zote  katika mchezo unaofuata utakaofanyika Desemba 27, 2025,  dhidi ya Uganda kabla ya kumalizana na Tunisia Desemba 30, 2025 ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kufuzu hatua ya mtoano.

Sanjari na hayo, Naibu Waziri Makonda amesema kikosi cha timu ya Taifa  Stars kipo bora tofauti na miaka ya nyuma, hivyo ametaka wachezaji kujituma ili kuongeza thamani yao na kuleta heshima kwa Taifa huku akiwasihi watanzania kuendelea kuiunga mkono na kuisemea vizuri timu hiyo.

"Hii michezo miwili iliyobaki tuhakikishe tunasogea mbele kwa kutoka kwenye hatua tuliyoishia mashindano ya 2023, tupande daraja kwa kufika hatua inayofuata ambayo ni mtoano", ameeleza Mhe. Makonda.

Aidha, amewahimiza kufanya vizuri ili wale wanaotegemea kustaafu waweze kustaafu kwa heshima na wale wanaoibukia waweze kutimiza ndoto zao kwa heshima ya kuivusha timu kwenda hatua nyjngine.

Taifa Stars ambayo inashiriki mara ya nne mashindano ya Afcon ipo kundi C na timu za Nigeria, Tunisia na Uganda, ambapo timu mbili zitakazofanya vizuri kila kundi zitakutana katika  hatua ya mtoano.
 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi