Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Makonda amesema amejiwekea dhamira ya kuifanya wizara hiyo kuwa mfano wa utendaji bora na kitovu cha ajira na ubunifu nchini.

Ametoa kauli hiyo leo Mei 16, 2026 jijini Arusha wakati akizungumza na wanahisa walioshiriki Mkutano Mkuu wa 31 wa Wanahisa wa CRDB Bank katika hafla ya 'Wanahisa Galla Dinner' iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).
Waziri Makonda amesema kuwa anatarajia wananchi wataona mabadiliko makubwa katika wizara hiyo ndani ya mwaka mmoja na endapo hilo halitatimia, yupo tayari kuwajibika.
“Huu ni mwezi wa tatu tangu nimekuwa Waziri katika Wizara yetu ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, mpango wangu ni kuhakikisha ndani ya mwaka mmoja kunakuwa na mabadiliko makubwa. Tusipoona mabadiliko hayo, mimi mwenyewe nitajiuzulu,” alisema Makonda.
Aidha, alisema ana malengo ya kuifanya wizara hiyo kuwa sehemu yenye kuvutia watumishi kutokana na mazingira bora ya kazi na fursa za maendeleo.

Alieleza kuwa ndani ya mwaka mmoja anatamani kuona watumishi kutoka wizara nyingine wakitamani kuhamia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kutokana na maboresho yatakayofanyika.
Makonda alisema wizara hiyo ina nafasi kubwa ya kuzalisha ajira, kukuza vipaji na kuondoa msongo wa mawazo kwa vijana kupitia sekta za habari, sanaa, michezo na utamaduni.
Katika hatua nyingine, Waziri huyo alisema serikali inaendelea kuvutia majina makubwa ya michezo duniani kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia michezo na utalii.
Amewashukuru wadau mbalimbali wakiwemo CRDB Bank pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa ushirikiano wao katika kufungua fursa za utalii na kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.