Mkutano wa 42 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika ngazi ya Makatibu Wakuu umefanyika leo tarehe 11 Juni 2022 katika Makao Makuu ya Jumuiya jijini Arusha.
Mkutano huo ambao umetanguliwa na mkutano wa Maafisa Waandamizi uliofanyika tarehe 8 na 9 Juni 2022 ulikuwa jukumu maalumu la kupokea na kupitia taarifa, agenda na mapendekezo yaliyotokana na Mkutano wa Maafisa Waandamizi kuhusu masuala mbalimbali ya Jumuiya na hatimaye, kuyawasilisha katika Mkutano wa Mawaziri utakaopangwa kufanyika baadaye mwaka huu.
Miongoni mwa masuala yaliyojiri katika mkutano huo ni uzingatiwaji wa ripoti mbalimbali ikiwemo ripoti ya kutoa mwelekeo wa kuanza kutumika kwa lugha ya Kifaransa na Kiswahili katika uendeshaji wa shughuli za kiofisi/rasmi za Jumuiya.
Katika Mkutano huo ujumbe wa Tanzania umeongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe
Viongozi wengine walioambatana naye ni pamoja na, Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Mary Makondo, Katibu Mkuu Afisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji –Zanzibar Bi. Khadija Rajab Khamis, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Amina Kh. Shaaban, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Mweli na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi. Wengine waliombatana naye ni Balozi Stephen P. Mbundi Mkurugenzi wa Siasa, Ulinzi na Usalama, Bw. Bernard Haule Mkurugenzi Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji na Bw. Eliabi Chodota, Mkurugenzi Idara ya Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii, wote wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja na Maafisa kutoka Wizara mbalimbali.
Mkutano huo uliofanyika kwa njia mseto (video na ana kwa ana) umehudhuriwa na nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ukiongozwa na Mwenyekiti wake Bw. Saitoti Torume CBS ambaye ni Katibu Mkuu,wa Hazina na Mipango kutoka Jamhuri ya Kenya
Baraza la Mawaziri ni chombo cha kutunga sera za Jumuiya. Baraza hilo linajumuisha Mawaziri wanaosimamia Masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki au Ushirikiano wa Kikanda.
Miongoni mwa majukumu ya Baraza la Mawaziri la Jumuiya ni kufuatilia na kufanya mapitio ya mara kwa mara juu ya utekelezaji wa programu za Jumuiya na kuhakikisha utendaji kazi mzuri wa Jumuiya.