[caption id="attachment_37031" align="aligncenter" width="750"] Ujumbe kutoka nchi mbalimbali za Jumuiya ya Afrika Mashariki, wakiwa katika kikao cha Makatibu Wakuu wa Nishati wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika Oktoba 18, 2018 jijini Arusha.[/caption]
Na Veronica Simba – Arusha
Makatibu Wakuu wa Wizara za Nishati wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, wamekutana jijini Arusha na kujadili miradi mbalimbali ya sekta husika, ikiwa ni sehemu ya Mkutano wa 13 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya hiyo.
Katika kikao hicho, Makatibu Wakuu wamepokea na kuidhinisha taarifa za wataalam wa sekta ya nishati kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambao wamekutana kwa siku tatu mfululizo kuanzia Oktoba 15, mwaka huu.
Miongoni mwa taarifa zilizoandaliwa na wataalam na kuidhinishwa na Makatibu Wakuu ni pamoja na zinazohusu sekta ndogo za nishati mbadala, uhifadhi wa nishati pamoja na ubora wa nishati.
Taarifa nyingine ni pamoja na ya sekta ndogo ya mafuta na inayohusu sekta ndogo ya umeme.
[caption id="attachment_37032" align="aligncenter" width="750"] Msimamizi wa uchimbaji madini katika Mgodi wa Dhahabu wa Sunshine uliopo katika kijiji cha Mbangala wilayani Songwe mkoani Songwe, Evarist Lukuba (kushoto) akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (wa tatu kushoto mbele) mara alipofanya ziara katika mgodi huo.[/caption]Dhima ya taarifa hizo zote ni kuboresha sekta ya nishati katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kuinua uchumi wa nchi husika, hivyo kuboresha maisha ya wananchi wake.
Awali, akiwasilisha salamu za ufunguzi wa kikao hicho cha Makatibu Wakuu, Naibu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Siasa, Charles Njoroge, akimwakilisha Naibu Katibu Mkuu wa Sekta za Uzalishaji na Jamii, alisisitiza umuhimu wa nchi wanachama kuendeleza jitihada za kuhakikisha kunakuwa na nishati ya uhakika, ya kutosha na ya bei nafuu katika eneo lote la Afrika Mashariki.
Aliongeza kwamba uhamasishaji wa miradi ya kuunganisha umeme inayotekelezwa kwa ushirikiano baina ya nchi wanachama, inayolenga kuvutia uwekezaji na kuhamasisha ushindani wa kibiashara katika nchi husika; ni moja ya vipaumbele vikuu vya sekta hiyo.
[caption id="attachment_37033" align="aligncenter" width="750"] Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Tanzania, Dkt. Hamisi Mwinyimvua (wa pili kutoka kushoto) pamoja na Makatibu Wakuu wenzake kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, wakitia saini taarifa inayohusu utekelezaji wa masuala mbalimbali ya sekta ya nishati katika nchi wanachama.[/caption]Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Maendeleo ya Madini wa Uganda, Robert Kasande, ambaye ni Mwenyekiti katika Ngazi hiyo ya Makatibu Wakuu, akifungua kikao husika, aliwataka wajumbe kutoa hoja na michango yenye mashiko itakayosaidia kuboresha zaidi sekta ya nishati katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kutoka Tanzania, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. Hamisi Mwinyimvua, ameshiriki kikao hicho.
Mkutano huo wa 13 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki, unatarajiwa kuhitimishwa kesho kwa Mawaziri husika kukutana, kujadili na kuidhinisha taarifa ya ngazi ya Makatibu Wakuu.