Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Makao Makuu Kikombo Yaakisi Ukomavu na Kujitegemea kwa Taifa
Feb 24, 2026
Makao Makuu Kikombo Yaakisi Ukomavu na Kujitegemea kwa Taifa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu katika hafla ya uzinduzi wa jengo la Makao Makuu ya Ulinzi Wa Taifa- kikombo-Dodoma
Na Baraka Messa- MAELEZO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, amezindua rasmi Makao Makuu ya Jeshi la Ulinzi wa Taifa (JWTZ) Februari 24, 2026 katika eneo la Kikombo, mkoani Dodoma, akieleza kuwa hatua hiyo ni alama ya ukomavu na uwezo wa Taifa kujitegemea katika kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati.

Rais Samia amesema ujenzi wa makao makuu hayo kwa kutumia fedha za ndani na wataalamu wa Kitanzania unaonesha dhamira ya dhati ya kuimarisha misingi ya uhuru wa maamuzi na heshima ya nchi kimataifa, hususan barani Afrika.

Amesisitiza kuwa majengo hayo yasibaki kuwa fahari ya miundombinu pekee, bali yawe nguzo imara ya kuimarisha ulinzi na usalama wa Taifa, sambamba na kusimamia misingi ya kitaaluma na nidhamu ndani ya jeshi.

Aidha, ameeleza kuwa makao makuu hayo yanapaswa kuwa kituo cha fikra na uchambuzi wa kisayansi kuhusu mikakati ya ulinzi, yakizingatia mabadiliko ya teknolojia na mazingira ya kiusalama duniani.

Rais Samia amebainisha kuwa katika zama hizi, ulinzi wa Taifa haujiegemezi kwenye silaha pekee, bali unahitaji ukusanyaji na uchambuzi wa taarifa, matumizi sahihi ya TEHAMA na mifumo madhubuti ya mawasiliano inayohitaji ubobezi wa hali ya juu.

Pia amesisitiza kuwa utii kwa mamlaka ya kikatiba na uaminifu kwa Taifa ni silaha kuu ya jeshi linaloheshimika, akiwataka wanajeshi kuendelea kuishi kwa misingi ya kiapo chao na kulinda heshima ya taasisi hiyo muhimu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Wananchi wa Tanzania (CDF), Jenerali Jacob John Mkunda, amesema ujenzi wa awamu ya kwanza wa makao makuu hayo umegharimu shilingi bilioni 121 na unaandika historia mpya tangu kuanzishwa kwa jeshi mwaka 1964, kwa kuwa sasa lina makao makuu ya kisasa yenye miundombinu bora na viwango vya juu vya kiusalama na kiutendaji.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi