Na Eleuteri Mangi-WUSM, Arusha
Makamu wa Rais wa Jumhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika ufunguzi wa Kongamano la Pili la Idhaa za Kiswahili duniani ambalo litafanyika kwa siku tano kuanzia Machi 14-18, 2022 katika Ukumbi wa Kimataifa (AICC) jijini Arusha.
Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw. Saidi Yakubu wakati wa mkutano na Waandishi wa Habari Machi 12, 2022 jijini Arusha ikiwa na maadalizi ya kuelekea ufunguzi wa kongamano hilo.
“Lengo la Kongamano hili ni kuwakutanisha pamoja Waandishi wa Habari na watangazaji wa Idhaa zote duniani zinazotumia lugha ya Kiswahili ili kuangalia wanavyotumia lugha hii katika shughuli zao za kihabari, kubainisha changamoto wanazokutana nazo na jinsi ya kuzitatua”, amesema Naibu Katibu Mkuu, Bw. Yakubu.
Hadi sasa washiriki kutoka vyombo vya habari mbalimbali vya ndani na nje ya nchi wamethibitisha kushiriki kongamano hilo ambapo zipo redio za hapa nchini 45, redio za nje 15, televisheni za kawaida na za mtandaoni 13, televisheni za nje ya nchi mbili, wahadhiri wa vyuo vikuu vya ndani 20, wachapishaji watano, watu mashuhuri kutoka ndani na nje ya nchi 16 pamoja na wanafunzi 200 kutoka vyuo vikuu vya jijini Arusha.
Washiriki hao wanajumuisha wawakilishi wa idhaa za Kiswahili za ndani na nje ya nchi, wataalamu wa Kiswahili na viongozi mbalimbali wa asasi za Kiswahili zinazojishughulisha na maendeleo na ufadhili wa shughuli za kukiendeleza Kiswahili.
Aidha, Kongamano ambalo litaangazia pia jitihada za vyombo vya habari katika ubidhaishaji wa lugha adhimu ya Kishwahili duniani na linatarajiwa kufungwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mpinduzi, Dkt Hussein Ali Mwinyi Machi 18, 2022.
Kwa upande wake Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Taifa, Bi. Consolata Mushi amesema kuwa kongamano hilo litakwenda sanjari na uzinduzi wa Kamusi Kuu ya Kiswahili Toleo la Tatu, uzinduzi wa mfumo wa kufundisha Kiswahili kwa wageni kwa njia ya mtanadao, uzinduzi wa kitabu cha matumizi ya TEHAMA katika tasnia ya Habari pamoja na uwasilishwaji wa mada 10 za kitaaluma kutoka kwa wahadhiri wa Vyuo Vikuu na wataalamu mbalimbali wa lugha ya Kiswahili
Washiriki wa Kongamano hilo wanatoka katika nchi za Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kenya, Malawi, Marekani, Rwanda, Ufaransa, Uganda, Ujerumani na wenyeji Tanzania.
Wazo la kuandaa Kongamano la Idhaa za Kiswahili Duniani lilianzishwa Novemba 29, 2006 na Kongamano la kwanza lilifanyika Novemba 12-15, 2007 ambapo lengo lake likiwa ni kuimarisha uhusiano na vyombo vya habari ambavyo vinatekeleza jukumu la kukieneza Kiswahili duniani kwa kukitumia na kutangaza katika vituo vyao vya habari.