Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Makamu wa Rais Azindua Mpango wa Tatu wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Fedha wa 2023-2028
Aug 03, 2023
Makamu wa Rais Azindua Mpango wa Tatu wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Fedha wa 2023-2028
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango akipokea kitabu cha Mpango wa Tatu wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Fedha wa 2023-2028 kutoka kwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Emmanuel Tutuba mara baada ya kuzindua mpango huo katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania Jijini Dar es salaam leo tarehe 03 Agosti, 2023.
Na Ofisi ya Makamu wa Rais

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema huduma jumuishi za fedha ni miongoni mwa vipaumbele vya nchi pia ni lengo muhimu la Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 pamoja na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano.

 

Makamu wa Rais amesema hayo wakati akizindua Mpango wa Tatu wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Fedha wa 2023-2028, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania jijini Dar es salaam.  Amesema huduma jumuishi za fedha ni nguzo muhimu inayopaswa kuzingatiwa kwa kuhakikisha watu wa makundi yote wanafikiwa.

 

Makamu wa Rais ametoa wito kwa wataalam na wadau wa huduma jumuishi za fedha kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuhakikisha wanaongeza kasi ya upatikanaji wa vitambulisho vya taifa ili kusaidia katika upatikanaji wa huduma rasmi za kifedha hususani kwa vijana. Aidha, amewasihi watalaam hao kuhakikisha malengo yaliowekwa katika mpango huo wa tatu wa huduma jumuishi za fedha yanafikiwa kikamilifu ifikapo mwaka 2028 hususani kwa kuelekeza juhudi katika makundi ambayo hayajafikiwa ikiwemo watu wenye ulemavu, wakulima wadogo, wavuvi, vijana, wanawake na wafanyabiashara wadogo.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango akihutubia wakati wa Uzinduzi wa Mpango wa Tatu wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Fedha wa 2023-2028, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania  Jijini Dar es salaam leo tarehe 03 Agosti, 2023.

 

Halikadhalika, Makamu wa Rais amesema ni vema kuendelea na jitihada za kuimarisha ulinzi wa watumiaji wa huduma za kifedha dhidi ya uhalifu wa mtandaoni ili kuwajengea wateja imani ya kuendelea kutumia huduma hizo. Pia ametoa rai ya kupunguzwa kwa gharama za kutumia huduma rasmi za kifedha pamoja na kuongeza wigo wa dhamana ili kurahisisha upatikanaji wa mikopo.

 

Makamu wa Rais ametoa wito wa kuongezwa na kurahisishwa kwa miundombinu ya malipo ya pamoja ili kuchochea matumizi ya huduma rasmi za fedha. Aidha, amesema ni muhimu kuhakikisha upatikanaji wa mawasiliano kwa wote ili kupunguza matumizi ya fedha taslimu.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wajumbe wa Baraza la Taifa la Huduma Jumuishi za Fedha mara baada ya kuzindua Mpango wa Tatu wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Fedha wa 2023-2028, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania  Jijini Dar es salaam leo tarehe 03 Agosti, 2023. (waliokaa kutoka kulia ni Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Emmanuel Tutuba, Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba, Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Albert Chalamila)

 

Kwa upande wake Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba amesema Mpango wa Tatu wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Fedha umeandaliwa kwa lengo la kuunganisha sekta binafsi na serikali ili kutatua changamoto za huduma jumuishi za fedha. Amesema mpango huo utasaidia kuongeza uelewa wa masuala ya huduma za fedha na kuongeza matumizi ya simu janja sambamba na kuhakikisha usalama wa wateja.

 

Dkt. Nchemba ametoa wito kwa wadau wa huduma jumuishi za fedha wa ndani na nje ya nchi kushirikiana wakati wa utekelezaji wa mpango huo wa tatu wa taifa ili kusaidia nchi iweze kupiga hatua katika kufikia malengo ya huduma jumuishi za fedha.

 

Awali akitoa taarifa kuhusu mpango huo, Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Huduma Jumuishi za Fedha ambaye ni Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Emmanuel Tutuba amesema utekelezaji wa mpango huo utaongeza upatikanaji wa vituo vya utoaji huduma za fedha katika maeneo ya vijijini, wigo mkubwa wa matumzi ya huduma za fedha kwa kuongeza machaguo na kuimarisha masuluhisho ya huduma kulingana na mahitaji ya wateja. 

 

Ameongeza kwamba, mpango huo unaunga mkono katika kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2025 na Dira ya Maendeleo ya Taifa Zanzibar ya Mwaka 2050, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano pamoja na mpango kabambe wa maendeleo ya sekta ya fedha ambao umeanza kutekelezwa mwaka 2020/2021-2029/2030.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi