Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe. Dkt. Emmanuel Nchimbi, amewasihi mabalozi wanaokwenda kuiwakilisha Tanzania katika mataifa mbalimbali kutanguliza mbele maslahi ya Taifa katika nyanja za kiuchumi, kisiasa na kidiplomasia.
Akizungumza na mabalozi hao wateule Ikulu Chamwino mkoani Dodoma alipokutana nao kwa lengo la kuwaaga, Dkt. Nchimbi amewahimiza wawe wabunifu na wachapakazi, huku wakitumia nafasi zao kutangaza fursa zilizopo nchini ili kuvutia wawekezaji na wafanyabiashara.

Aidha, amewataka mabalozi hao kusimamia maono ya Samia Suluhu Hassan katika juhudi za kujenga uchumi na kuimarisha uhusiano wa kimataifa.
Makamu wa Rais amesisitiza umuhimu wa mabalozi hao kuzingatia na kusimamia Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi pamoja na miongozo mbalimbali ya Serikali katika utekelezaji wa majukumu yao.

Vilevile, amewapongeza kwa kuaminiwa na Rais kwenda kuiwakilisha Tanzania katika mataifa mbalimbali na kuwataka kutumia vyema nafasi hiyo kwa manufaa ya Taifa.
Akizungumza kwa niaba ya mabalozi hao, Balozi mteule wa Tanzania nchini Oman, Maulidah Hassan, amemshukuru Makamu wa Rais kwa maelekezo na ushauri aliotoa, na kuahidi kuwa watafanya kazi kwa bidii kutekeleza majukumu yao.

Mabalozi hao wateule ni pamoja na Zena Ahmed Said (Saudi Arabia), Cyprian Luhemeja (Zambia), Maulidah Hassan (Oman), Salim Othman Hamad (Comoro), Swahiba Mndeme (Sweden), Noel Kaganda (Korea), pamoja na Musa Haji Ali