Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango leo tarehe 31 Mei 2022 amewasili Stockholm nchini Sweden ambapo anatarajia kuhudhuria mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Stockholm +50 utakaofanyika tarehe 2 hadi 3 Juni 2022 nchini humo.
Dhumuni la mkutano huo ni kuchochea utekelezaji wa Malengo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (Ajenda 2030) hususan katika upande wa mazingira na kujadili namna ya kurejesha uchumi endelevu katika kukabiliana na janga la Uviko 19.
Aidha, mkutano huo ni maadhimisho ya miaka 50 tangu kufanyika mkutano wa kwanza wa mazingira wa Umoja wa Mataifa uliofanyika mjini Stockholm mwaka 1972.
Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Stockholm +50 unahudhuriwa na Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka mataifa mbalimbali pamoja na wadau wa Mazingira Duniani.